Na Peter Mwenda
WASANII wa dansi na kizazi kipya nchini wametakiwa kujiendeleza kwa kusomea fani hiyo kwa sababu ni ajira iliyo wazi kupata kazi duniani kote.
Mkurugenzi wa Music Empowerment Trust (MET), Angelo Luhala akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vyeti kwa wasanii 16 waliomaliza masomo ya kupiga kinanda, kupiga saxaphone,kupiga gita na kuimba katika chuo cha Alphabeta cha Tabata Liwiti, Dar es Salaam juzi alisema wasanii wana nafasi ya kufanya kazi sehemu yoyote duniani kama watakuwa wamesomea kazi hiyo vyuoni.
"Sasa tuachane na kupiga muziki wa mitaani, jifunzeni kupiga muziki wa kusomea kutumia nota,kuna wanamuziki wa Tanzania waliitwa kwenda kupiga muziki Kenya, walipofika walipewa nota na kukabidhiwa vyombo wapige muziki kwa sababu walikuwa hawajui kutumia nota, waliondoka kimya kimya kurudi nchini, watanzania futeni aibu hii" alisemaLuhala.
Alisema chuo cha Alphabeta ni mkombozi kwa wasanii watanzania ambao wanatakiwa kuanza kusoma muziki wa darasani na vitendo ili wapige muziki kuongozwa na nota badala ya kujifunza kupiga muziki mitaani na kuridhika wao ni wanamuziki.
Katika mahafali hayo msanii Edwin Mrope aliibuka kuwa mwanafunzi bora baada ya kujifunza na kupiga vyombo vyote vya muziki katika kipindi cha mwaka mmoja wa masomo yake.
Awali Mkurugenzi wa Alphabeta, Mark Manji alisema kutoka chuo hicho kifunguliwe mwaka jana idadi ya wanafunzi wanaojiunga kusomea fani hiyo inazidi kupungua kutokana na sababu mbalimbali lakini kubwa ni ya kushindwa kupata ada ya masomo.
Manji alisema lengo la chuo hicho ni kutoa elimu ya muziki kwa watanzania ili waweze kumudu kufanya kazi nchi mbalimbali duniani ambako wasanii wanapata ajira na kulipwa fedha nyingi kwa kazi ya muziki.
Alisema kuna fani ambazo zimeanza kutoweka kama ya wapiga saxaphone na tarumbeta ambao sasa wamebaki wachache kwenye bendi za mitaani na bendi za majeshi hivyo alitoa wito kwa vijana wanaopenda muziki kujifunza kupiga vyombo hivyo.
Wanafunzi wa fani ya muziki kama ilivyo michezo wanatoka katika familia za kimasikini na hiyo kushindwa kupata ada ya kulipia masomo yao hata wale wanaofanya kazi wanashindwa kutoa mishahara yao kusomea muziki.
Alisema kutokana hiyo asilimia 75 wanasitisha masomo yao kutokana na kushindwa kupata fedha za kulipia ada ya kusomea muziki na kuwafanya wanamuziki wengi kupiga muziki bila kuusomea.
mwisho.
No comments:
Post a Comment