TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Monday, 23 April 2012

MKUTANO MKUU WA MWAKA 2011 WA TFF
Mkutano Mkuu wa Mwaka (AGM) wa 2011 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umefanyika kwa siku mbili (Aprili 21-22 mwaka huu) kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront na kuhudhuriwa na wajumbe 104. Mkutano ulipokea taarifa, kufanya uamuzi katika masuala mbalimbali na mengine yaliyojitokeza kama ifuatavyo;
 
EL MAAMRY, NDOLANGA WATUNUKIWA URAIS WA HESHIMA
AGM ilipitisha pendekezo la kuwatunuku urais wa heshima wa TFF, Alhaji Said Hamad El Maamry na Muhidin Ahamadi Ndolanga lililowasilishwa na Mwenyekiti wa mkutano huo ambaye pia ni Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
 
Alhaji El Maamry ambaye ni mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) alikuwa Mwenyekiti wa TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) kuanzia mwaka 1973 hadi 1986. Alhaji Ndolanga aliongoza FAT kuanzia mwaka 1993 hadi 2004.
 
BAJETI YA MWAKA 2012
Bajeti ya Mwaka 2012 ya sh. 7,246,628,650 kwa ajili ya matumizi ya TFF ilipitishwa. Kwa mwaka 2012 TFF inatarajia kukusanya sh. 7,572,991,433 kupitia vyanzo mbalimbali.
 
Vyanzo hivyo ni viingilio vya uwanjani vinavyotarajiwa kuingiza asilimia 22 ya mapato yote, udhamini (asilimia 74) na vyanzo vingine kama haki za matangazo ya televisheni, ada za ushiriki wa timu katika mashindano mbalimbali, misaada kutoka FIFA na CAF ambayo kwa pamoja vinatarajiwa kuingiza asilimia nne ya mapato yote.
 
KAMATI YA LIGI YA TFF
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itaendelea na mchakato wa kupendekeza mifumo mitatu tofauti ya chombo kitakachosimamia/kuendesha Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ikieleza faida na athari za kila mfumo uliopendekezwa na baadaye kuwafanya mawasilisho (presentation) kwenye Kamati ya Utendaji.
 
Baada ya kuwasilisha mifumo hiyo kwa Kamati ya Utendaji, Kamati ya Ligi itapendekeza mfumo upi kati yao hiyo inaoona unafaa kabla ya kufanyika uamuzi wa mwisho.
 
Lengo la kuunda chombo maalumu cha kuendesha ligi ni kuongeza ufanishi katika uendeshaji wa VPL na FDL, na pia kuifanya Sekretarieti ya TFF kushughulikia zaidi shughuli za maendeleo.
 
UUZWAJI WA TIMU
Uuzaji wa timu linabaki kuwa suala la kisheria. Lakini TFF imeweka utaratibu ufuatao; lazima Mkutano Mkuu wa klabu husika uidhinishe uuzaji, na timu ikishauzwa inabaki katika mkoa husika.
 
MFUMO WA MASHINDANO
Kwa vile kuna tatizo la ligi mbalimbali kuwa fupi, hali inayosababisha baadhi ya wachezaji katika madaraja ya chini kucheza ligi zaidi ya moja katika msimu mmoja, mfumo wa ligi/mashindano utaangaliwa upya.
 
Mfumo uliopo sasa uliwekwa kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika mpira wa miguu ambapo mwekezaji anaweza kuanzisha timu, na ndani ya miaka mitatu ikacheza Ligi Kuu. Pili, ilikuwa ni kuondoa mlolongo mrefu wa ligi, na kuwafanya wanachama wa TFF (mikoa) nao kuendesha ligi zao mikoani.
 
Ijulikane kuwa ligi za mikoa (regional leagues) zinachezwa. Kwa sababu TFF inaendeshwa kwa mfumo wa shirikisho (federation), nia ni wanachama wa federation nao kuwa na majukumu ya kusimamia na kuendesha ligi, kwa vile TFF haiwezi kusimamia ligi zote.
 
MAREKEBISHO YA KATIBA
Mkutano Mkuu wa TFF umepitisha marekebisho ya Katiba katika maeneo mawili; moja ni kuanzisha Baraza la Wadhamini ambalo linatakiwa kuwa na wajumbe wasiopungua watatu na wasiozidi watano.
 
Marekebisho mengine ni kuongeza idadi ya kanda kutoka kumi na moja za sasa hadi 13. Marekebisho hayo yamefanyika kutokana na Serikali kuongeza mikoa mipya ya kijiografia.
 
Kanda mpya sasa zitakuwa Kagera/Geita, Arusha/Manyara, Kilimanjaro/Tanga, Katavi/Rukwa, Njombe/Ruvuma, Dodoma/Singida, Dar es Salaam, Shinyanga/Simiyu, Mwanza/Mara, Lindi/Mtwara, Kigoma/Tabora, Mbeya/Iringa na Pwani/Morogoro.
 
Ukiondoa mamlaka ya uteuzi aliyonayo Rais kwa mujibu wa Katiba ya TFF, wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji huchaguliwa kwa kanda.
 
HESABU ZILIZOKAGULIWA
Mkutano Mkuu ulipitisha hesabu zilizokaguliwa za mwaka 2010 (Audited Accounts) , na pia kuiteua kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya TAC Associates kuwa mkaguzi wa hesabu za TFF kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
 
YANGA YAOMBA RADHI MKUTANO MKUU
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ambaye pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF akiwakilisha klabu za Mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Bhinda aliwaomba radhi wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kitendo cha wachezaji wake kumpiga mwamuzi Israel Nkongo kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu.
 
Pia alimuomba Rais wa TFF, Leodegar Tenga kutoa msamaha wa adhabu ya kulipa faini iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa wachezaji wawili wa Yanga ambao mpaka sasa hawajalipa faini hiyo.
 
Rais Tenga alimshukuru Bhinda kwa ujasiri alioonesha wa kuomba radhi mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kitendo kile. Aliongeza kuwa kwa vile yeye ni muumini wa kanuni, na adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni hawezi kutoa msamaha, hivyo wachezaji hao walipe faini hizo.
 
Pia Rais Tenga alisema binafsi haziingilia kamati za TFF katika uamuzi ambao zinafanya kwa vile zina watu waadilifu, na angekuwa yeye binafsi ndiye anayetoa adhabu, angetoa adhabu kali zaidi kwa vile vitendo vya kupiga waamuzi havikubaliki katika mchezo wa mpira wa miguu.
 
KANUNI ZA NIDHAMU, MAHAKAMA YA USULUHISHI
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Rais Tenga aliwaambia wajumbe kuwa Kanuni za Nidhamu (Disciplinary Code) za TFF na uundaji wa Mahakama ya Usuluhishi (Arbitration Tribunal) ya TFF ambacho ndicho kitakuwa chombo cha juu cha kutoa haki kwa masuala ya mpira wa miguu nchini vitakamilika mwaka huu.
 
Pia TFF itaendelea kutafuta wadhamini kwa ajili ya timu za Taifa za vijana na wanawake, itaendelea kuendesha semina na makongamano katika nyanja mbalimbali za mpira wa miguu, kutengeneza mtaala wa academy na kutengeneza mpango wa maendeleo (Comprehensive Plan) baada ya ule wa awali kumalizika mwaka huu.
 
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment