TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Thursday, 27 October 2011

Jiji la Dar es Salaam lanunua mashine ya kushindilia taka Pugu Kinyamwezi

Na Peter Mwenda

MIKAKATI ya Jiji la Dar es Salaam kutumia takataka za dambo la Pugu Kinyamwezi kuzalisha umeme, gesi na kuondoa kero ya harufu mbaya kwa wananchi wa eneo hilo zimeanza kuonekana baada ya kununua mashine yenye thamani ya dola 4.5 kwa ajili ya kushindilia takataka zinazozalishwa.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dkt. Didas Masaburi akizungumza baada ya kukabidhiwa mashine hiyo na Kampuni ya Manrac ya jijini Dar es Salaam juzi alisema fedha za kununulia mtambo huo ni mkopo wa Benki ya Uwekezaji (TIB) ambazo zitalipwa ndani ya miaka mitano.

Alisema Jiji la Dar es Salaam linapanga mikakati ya kukopa fedha ambazo zitatumika kubadilisha matumizi ya dampo la Pugu Kinyamwezi kuwa kitegauchumi kwa kuzifanya takataka hizo zishindiliwe vizuri na kuhifadhiwa ili zizalishe umeme na gesi.

Alisema kwa kuanzia wamefanya mazungumzo na Benki ya Dunia ambao wameonesha uwezekano wa kutoa fedha hizo zitakazotumika kufanya kazi hiyo ambayo imewezekana katika majiji ya nchi nyingine duniani.

Bw. Masaburi akizungumzia mashine hiyo alisema kwa kuanzia itasaidia kupunguza gharama walizokuwa wanazipata awali za kukodi mashine kwa ajili ya kazi hiyo kwa vile zile za Jiji zilikuwa zimechoka na kutumia mafuta mengi.

Alisema Jiji la Dar es Salaam ambalo huzalisha taka nyingi kuliko majiji mengine nchini, mashine hiyo itasaidia kushindilia na kuziteketeza taka taka hizo na kushauri kampuni zinazozoa taka kupeleka kwa wingi.

Ofisa Masoko wa kampuni ya Mantrac, Bw. Olais Ole Lobove alisema mashine hiyo inauwezo wa kufanya kazi saa 24 bila kupumzika na kuahidi kampuni yao kutoa msaada wa kiufundi wakati wowote unapohitajika na kutoa garantii ya mwaka mmoja wa kubadilisha mashine hiyo iwapo itapata hitilafu.

Mapema mwaka huu wananchi waishio karibu na dampo la Pugu Kinyamwezi walilalamikia harufu mbaya inayotoka katika dampo hili hasa kipindi ambacho mvua zimenyesha na ilifika wakati kutishia kuandamana.

mwisho

No comments:

Post a Comment