TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Thursday, 11 August 2011

Dkt Masaburi amwaga ugali. avunja Bodi ya Mtemvu DDC

Na Peter Mwenda

MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Dkt. Didas Masaburi amevunja Bodi ya Shirika la Uchumi na Maendeleo Dar es Salaam (DDC)ambalo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Temeke, Bw. Abbas Mtemvu baada ya kugundua udhibiti hafifu wa mali za shirika hilo na mikataba ya kiujanja ujanja.

Katika ziara ya ghafla ya Meya Dkt. Masaburi aliyoifanya jana katika miradi ya DDC Kariakoo, DDC Magomeni na DDC Mlimani Park, Dkt. Masaburi aligundua kuwa mikataba ya maduka ya Kariakoo imekuwa ikiwanufaisha wachache na Jiji kuambulia patupu.

Katika maduka aliyotembelea ambayo wafanyabiashara wake ni kutoka China na wengine watanzania katika duka la kwanza alikuta mmiliki wa kwanza amemkodishia mtu mwingine kwa gharama ya juu wakati yeye akilipa DDC fedha kidogo.

Duka mojawapo ambalo mmiliki wake ni Mchina analipa kodi ya sh. mil. 1.6 wakati DDC inalipwa sh. 300,000 tu na duka la pili pia ambako kuna mchina analipa sh. mil. 2.6 hali DDC ikipokea sh. 300,000.

Wakati akienelea na ziara hiyo alimkuta mmoja wa wajumbe wa Bodi, Bw. Jerome Bwanausi akiwa katika mmoja ya maduka ya DDC ambako alimweleza bayana kuwa bodi yao imekuwa ikikodisha maduka ya DDC kwa bei kubwa hali wakilipa kodi ya sh. 300,000 tu.

Bw. Bwanausi ambaye ni Mbunge wa Lulindi hakupata nafasi ya kueleza zaidi huku akiwa amezungukwa na waandishi wa habari alionesha kumsikiliza bila ya kusema kitu zaidi na baadaye kurudi dukani hapo kwa shughuli zake huku ziara hiyo ikiendelea.

Dkt.Masaburi aliwataka wenye maduka hayo watoe ushirikiano kwa Kaimu Meneja wa DDC, Bw. Cyprian Mbuya ambaye amempa siku saba akusanye mikataba yote ya maduka 80 yanayuzunguka DDC Kariakoo na mingine ta Keko, Magomeni na Mlimani.

Kaimu Meneja Bw. Mbuya alikitoa taarifa ya hali ya shirika hilo alisema mpaka sasa linadaiwa sh. mil. 500 na kila mwezi linaingiza jumla ya sh. mil.46.6 kwa mwezi kutokana na kupangiosha ofisi, maduka 75, mgahawa na baa ambayo ni sawa na sh. 559.7 kwa mwaka.

Dkt. Masaburi alisema endapo kutakuwa na uthibiti wa mali za shirika hilo maduka ya Kariakoo peke yake yanauwezo wa kuingiza sh. mil. 600 kwa mwaka lakini kwa sasa inaingiza fedha kidogo na nyingine kuingia kwenye mifuko ya watu hivyo Jiji ambao ni wamiliki kwa asilimia 100 haijapata gawio kwa miaka mingi iliyopita.

Katika mradi wa DDC Magomeni Dkt. Masaburi alishudia gereji ambayo iko katika mgogoro na shirika hilo kwa miaka mingi na kuwashauri wakae pamoja na kuafikiana ili pande zote zinufaike.

Mkurugenzi Msaidizi wa gereji hiyo Bw. Juma Salum alisema yuko tayari kumaliza tofauti hizo kwani wanaushirikiano mkubwa na Jiji kwa vile magari yote ya halmashauri yanatengenezwa kwenye gereji hiyo.

Awali Kaimu Meneja Miradi na Ugavi Bw. Rupia John alisema ni kweli kuna utata wa mali na vifaa walivyokabidhiwa wakati wakiingia madarakani kwani katika kiwanja ambayo Dkt. Masaburi alisema ni mali ya Jiji hawana taarifa zake.

Dkt. Masaburi alikuwa na orodha hiyo aliwaonesha kuwa ofisi inayotumika na Kampuni ya Udalali ya Majembe kitalu namba 2289 iliyoko mtaa wa Nkurumah ni mali ya DDC na kuna kiwanja kingine namba 1 mtaa wa Azikiwe na Indira Ghandi ambako iko sheli ni mali ya shirika hilo.

Aliwataja wajumbe wa Bodi aliowavua madaraka kuwa ni Mwenyekiti wao Bw. Mtemvu na Wajumbe ni Mbunge wa Lulindi Bw. Jarome Bwanausi, Bw. William Bomani, Bi. Rehema Mayunga,Bw. Wendo Mwapachu na Isaac Tasinga.

Shirika la DDC lina miradi ya shamba la Ruvu lenye ekari 10,000, Shamba la Malolo lenye ekari 5,000, miradi ya DDC Kariakoo, DDC Keko, DDC Mlimanni Park, DDC Magomeni na Parval Garage ya Magomeni.

mwisho

No comments:

Post a Comment