Na Peter Mwenda
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw. Emmanuel Nchimbi ameongoza maelfu ya waombolezaji kuaga mwili wa Naibu Mhariri wa New Habari 2006 Ltd, Danny Mwakiteleko kabla ya kusafirishwa kuzikwa nyumbani kwao Tukuyu, Mbeya.
Katika salamu za rambirambi za Kampuni ya New Habari 2006 Ltd imeahidi kumlipa mke wa marehemu Mwakiteleko mshahara ya kila mwezi kwa miaka mitano, kusomesha watoto wake wawili na watoto wa marehemu kaka yake hadi Chuo Kikuu.
Mtendaji Mkuu wa New habari 2006 Ltd, Bw. Hussein Bashe alisema mtoto wa kwanza wa marehemu Mwakiteleko anayosoma kitado cha tatu na mdogo wake anayesoma darasa la sita watapewa heshima kama baba yao alivyoifanya kazi kwa uadilifu katika kampuni hiyo.
Bw. Bashe alisema Mwenyekiti Mtendaji wa New Habari 2006 Ltd, Bw. Rostam Aziz ameahidi kuiangalia familia hiyo kwa karibu ikiwemo kuwasomesha watoto wawili wa kaka yake Mwakiteleko aliokuwa akiishi nao hadi elimu ya chuo Kikuu.
Alisema marehemu Mwakiteleko alikuwa msikivu, mwajibikaji na mchapa kazi na kabla ya kifo chake alikuwa akiandaa toleo maalum la miaka 50 ya Uhuru.
Jukwaa la wahariri katika salamu zao zilizosomwa na Bw. Manyerere Jackton zilisema marehemu ameacha funzo kubwa kwa wanahabari kujituma kwani kwa namna ya pekee marehemu anastahili kupata waombolezaji wengi kama walivyokuwa jana kutokana na tabia yake ya kupenda kazi.
Katika salamu mbalimbali zilizotolewa Waziri Nchimbi aliyemwakilisha Rais Kikwete alisema amesikitishwa na kifo hicho na kuahidi Ikulu kutoa mkono wa pole kwa familia hiyo.
Wengine walitoa rambirambi zao ni Jukwaa la Wahiriri sh. 3.320,000, CRDB sh. mil. 1, NHC sh. 700,000, PPF sh. 500,000, Jeshi la Polisi Tanzania sh. 200,000 Kamati ya Nishati na Madini sh. 500,000 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Benard Membe alitoa sh. 200,000 na Sport FM ya Dodoma sh. 100,000 na TANESCO sh. 500,000.
Wakati huo huo Chama cha Waandishi wa Habari wanawake (TAMWA) kimemwelezea marehemu Mwakiteleko kuwa alitumia nafasi yake kuchapisha habari bila ubaguzi wa kijinsia.
Alisema TAMWA itaendelea kumkumbuka marehemu Danny kutokana na moyo aliokuwa nao wa kushirikiana na watetezi wa haki za binadamu katika harakati za kukomesha ndoa za utotoni na mimba za za mashuleni ambazo zinakwamisha watoto wa kike kupata elimu.
Marehemu Mwakiteleko alifariki Jumatato iliyopita saa 4 usiku katika eneo la TOT, Tabata baada ya kukonga lori kwa nyuma wakati akitokea kazini kwenda nyumbani kwake Tabata Chang'ombe.
Mwili wa marehemu Mwakiteleko utasafirishwa kwenda Mwakaleli Tukuyu Mbeya ambako anatarajiwa kuzikwa leo. Ameacha mke na watoto wawili. Mungu ilaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amen.
mwisho
No comments:
Post a Comment