TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Friday, 8 July 2011

Msajili amuru uchaguzi CHAWATIATA ndani ya siku 30

Na Peter Mwenda

MSAJILI wa Vyama wa Wizara ya Mambo ya Ndani ameamuru viongozi wa Chama cha Waganga na Wakunga wa Tiba Asilia Tanzania (CHAWATIATA)kufanya Uchaguzi Mkuu ndani ya siku 30.

Katika barua aliyowaandikia viongozi hao ya Julai Mosi mwaka huu iliyosainiwa na Bw. Seperatus Fella pia imetengua adhabu ya kufutiwa uanachama Mwenyekiti wa CHAWATIATA Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Maneno Tamba na viongozi wenzake.

Bw.Fella alisema tarehe ya kufanyika uchaguzi huo itolewe kwa Msajili wa Vyama na baada ya uchaguzi kufanyika taarifa ifikishwe wizarani ndani ya siku 14.

Alisema Mwenyekiti wa CHAWATIATA Taifa Bw. Selemani Ruwa na Katibu wake Bw. Mittan Magombeka wamekihujumu chama kwa makusudi kwa kushindwa kulipa ada ya mwaka kwa Msajili kwa muda wa miaka mitatu mfululizo ambazo ni jumla sh. 200,000 na kusababishja wanachama kuchangishana ili kukinusu chama chao na kuzilipa.


Msajili huyo alisema hata baada ya kuitisha vikao mara mbili vya usuluhishi kati ya uongozi wa taifa CHAWATIATA na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam Bw. Magombeka na Mwenyekiti wake hawakuhudhuria hivyo ametoa uamuzi wa upande mmoja.

Alisema Mwenyekiti wa mkoa wa Dar es Salaam,Bw. Tamba na wenzake ambao walifutiwa uanachama wao na viongozi wa kitaifa wamerejeshewa kwa sababu viongozi wa CHAWATIATA taifa si halali.

Alisema viongozi wa CHAWATIATA si halali kwa sababu kwa miaka 16 walitakiwa kurekebisha katiba lakini hawajafanya hivyo muda wa uongozi kukaa madarakani ni miaka minne ambao ulikwishapita muda mrefu na wao bado wanaendelea kuongoza bila kuitisha uchaguzi.

Viongozi walifutiwa uanachama wao ni Bw. Tamba, Bw. Sunna Mkote, Bruno Namanga na Lily Mwikkoki ambao walikuwa viongozi wa CHAWATIATA Mkoa wa Dar es Salaam.

Katibu wa CHAWATIATA, Bw. Magombeka alipotafutwa kutoa msimamo wake, simu yake ya mkononi haikupokelewa.

mwisho

No comments:

Post a Comment