Na Peter Mwenda
WATU wawili wanaosaidikiwa kuwa majambazi wamepora fedha za Kampuni ya Simu ya Mkononi Airtel katika tukio lililofanyika hatua chache kutoka ilipo ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Said Mwema.
Dereva wa gari la Airtel, Bw. Francis Kilewo na Mhasibu Idd Ndee wakiwa katika gari T 450 ATD wakitoka Makao makuu ya kampuni hiyo, Morocco walijikuta wanazingirwa na watu wawili wakiwa na bastola mbili na kunja kioo cha gari upande alipokuwa amekaa Mhasibu Ndee.
Katika tukio hilo lilitokea jana mchana saa 7.45 (saa saba na robo), dereva wa gari hilo akiwa amesimama katika makutano ya barabara ya Uhio na Ghana mita chache kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ilisikika milio ya bastola iliowafanya polisi kukimbilia eneo la tukio lakini tayari majambazi hayo yalikuwa yamepora fedha na kukimbia kutumia pikipiki.
Dereva wa gari hilo,Bw. Francis Kilewo akisimulia tulkio hilo alisema alishtuka kioo cha gari hilo upande aliokaa Mhasibu kimevunjwa na kuwekewa bastola kichwani.
Alisema naye alijikuta naye amenyoshewa bastola na jambazi mwingine alimtaka afungue dirisha la upande wake lakini hakutii amri hiyo ndipo alitwangwa tofali mkononi.
Bw. Kilewo akiendelea kusimulia mkasa huo alisema Mhasibu aligoma kutoa fedha hizo ndipo jambazi mmoja alipopiga risasi juu lakini hata hivyo Bw. Ndee aligoma kuzitoa na kunyang'anyana kwa nguvu.
Mwandishi wa habari hizi aliyekuwa karibu na tukio hilo aliona askari wa wizara ya Mambo ya Ndani, polisi wa doria na wapelelezi wakizunguka gari hilo na kuwahoji dereva na Mhasibu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Bw. Faustine Shilogile alipoulizwa kuthibitisha tukio hilo aliahidi kutolea taarifa baada ya kutoka mkutanoni.
mwisho
No comments:
Post a Comment