Na Peter Mwenda
SAKATA la wakazi wa Tanganyika Packers, Kawe kudai kuvuta hewa ya dawa zenye kemikali limeingia katika hatua nyingine baada ya Mwenyekiti wa mtaa wa Mzimuni Bw. Hassan Ngonyani kumkana Diwani wa Viti Maalum Chadema Bi. Ester Samanya kuwa hahusiki na eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Bw. Ngonyani alisema diwani huyo ni wa Kata ya Mikocheni hivyo hapaswi kuingilia mambo ya Kata ya Kawe kwani anatumia propaganda za kisiasa zenye uongo ndani yake na kupaka matope uongozi wa mtaa wake.
Akiwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo walimtaka diwani huyo kuacha kuingilia mambo ya mtaa wa Mzimuni Bw. Ngonyani alisema amegundua kuwa Chadema imeanzisha propaganda ya kuipaka matope CCM.
Alisema Diwani Samanya hajawahi kufika katika mtaa wake kujitambulisha bali amekuwa akipita huku na huko kutangaza kuwa takataka za sumu zilizimwagwa dampo la Kawe zimetokana na uongozi wake jambo ambalo linajenga chuki na kumchonganisha na wananchi wake.
"Hata Mbunge wa Kawe, Bi. Halima Mdee hatushirikishi katika vikao vyake na wananchi, utasikia mbunge yupo anazungumza na wakazi wa sokoni bila kutoa taarifa kwa viongozi wa mtaa, huo si utendaji kazi unaotakiwa kwa ajili ya kutumikia wananchi" alisema Bw. Ngonyani.
Naye Diwani wa Viti Maaalum Kata ya Kawe, Bi. Samanya alipopigiwa simu kuhusu shutuma hizo alisema wadhifa wake unamruhusu kufanya kazi katika jimbo lote la Kawe.
Alisema aliomba nafasi hiyo kupitia jimbo la Kawe lakini ni diwani wa Jimbo lote la Kawe kupitia Chadema na atafanya kazi za kutumikia wananchi bila woga hasa pale atakapoona hakuna utendaji wa kuwajibika kwa wananchi.
Akizungumzia kemikali za dambo hilo, Bi. Ester alisema kitendo cha watu kumwaga mapipa ya madawa yenye sumu na kuyachoma eneo la makazi ya watu ni makosa ambayo hayawezi kufimbiwa macho.
Majira ilirudi tena eneo la dampo hilo na kukuta mapipa ya madawa yenye kemikali hayo yakiwa yamefunikwa maturubai ya kuzuia harufu kali ili zisiendelee kuathiri wakazi wa eneo hilo.
mwisho
.
No comments:
Post a Comment