TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Saturday, 18 December 2010

Ilala, Kisarawe kubaki gizani hadi Jumanne

Na Peter Mwenda

TRANSIFOMA la Shirika la Umeme (TANESCO) la Kipawa jijini Dar es Salaam lilioharibika na kusababisha umeme kukosekana katika maeneo mengi ya wilaya ya Ilala Dar es Salaam na Kisarawe mkoa wa Pwani litakamilika na kuanza kufanya kazi Jumanne ijayo.

Meneja wa Mradi wa Kampuni ya National Contracting Co. Ltd ya Saudi Arabia inayofunga transifoma hiyo, Bw. Sadeesh John alisema kazi ya kufunga transifoma hiyo imekamilika bali bado kujaza mafuta na kukamilisha uunganishaji wa nyaya.

Alisema kumalizika kufunga transifoma hilo na kuanza kazi kutategemea kama mvua hazitanyesha kuathiri utendaji wa kazi vinginevyo hakutakuwa na mabadiliko mengine.

Bw. Sadeesh alisema kuchelewa kufunga transifoma hiyo kumetokana na sababu mbalimbali hasa pale ilipotumika muda mrefu barandarini katika kitengo cha ushuru wa Forodha wakati wa kuondosha vipuri vya transifoma hiyo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Alisema transifoma hiyo iliyotengenezwa nchini India yenye uwezo wa kupokea msongo wa umeme wa Voltage 45 inachukua nafasi ya jingine la Italia ambalo limeharibika.

Transifoma hilo liliharibika mapema mwezi uliopita na kusababisha maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam kukosa umeme kwa zaidi ya saa 16 na kusababisha huduma na uzalishaji mali kushuka.

Kati ya walioathirika zaidi ni wagonjwa katika hospitali ya Kisarawe mkoani Pwani ambao wameshindwa kufanyiwa upasuaji kwa kukosa maji yanayozalishwa na umeme.

Meneja Uhusiano wa TANESCO, Bi. Badra Masoud aliwaomba wakazi wa maeneo hayo kuvuta subira wakati kazi ya kumalisha ufungaji wa transfoma unakamilika.

mwisho.

No comments:

Post a Comment