TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Friday 26 June 2015

Nyambui asikitikia michezo Tanzania

Na Peter Mwenda

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) aliyeachia wadhifa huo, Suleiman Nyambui ameiasa Serikali kuwa ikitaka kurudisha heshima ya michezo kama zamani ni lazima irudishe vipindi vya michezo (Physical Education PE) kuanzia shule za msingi.

Nyambui ambaye amejing'atua kuendelea na madaraka yake ya Ukatibu Mkuu wa RT baada ya kuingia mkataba wa kufundisha riadha kwa kipindi cha miaka miwili nchini Bunei barani Asia, alisema Tanzania kama haitarudisha michezo katika programu zake hakutakuwa na ushindi.

Alisema Serikali ikiweka mikakati ya michezo na kutenga viwanja vyenye ubora vya kuchezea tutaendelea kuwa wasindikizaji katika michezo yote ya riadha, soka, netiboli, ngumi na mingine.

Nyambui alisema Tanzania imejaliwa kuwa na baadhi ya maeneo yanayofaa kwa ajili ya kujenga viwanja na kuweka kambi za mazoezi kwa timu za taifa kama Tanga,Mbulu, Arusha, Singida, Njombe, Makambako na Mbeya ambako hali ya hewa inaruhusu wachezaji kufanya mazoezi kwa nguvu.

Alisema kutofanyika mashindano ya michezo katika ngazi za wilaya inawanyima wachezaji wengi wenye vipaji kuonesha uwezo wao wa kujituma kutumikia taifa katika michezo kwa sababu hawaonekani.

Akipokea zawadi ya suti na vifaa vya michezo vyenye bendera ya Taifa kutoka Kampuni ya Isere Sports, Nyambui alisema Serikali pia inatakiwa kuwasaidia waagizaji na wauzaji wa vifaa vya michezo wapunguziwe ushuru ili wauze vifaa hivyo kwa bei nafuu.

Nyambui aliyewahi kuwa mshauri wa ununuzi wa vifaa vya michezo wa Kampuni ya Isere alisema katika kipindi cha miaka miwili atakayokuwa nje ya Tanzania bado ataendelea kutoa ushauri kwa watanzania wa njia nzuri ya kujikwamua.

mwisho 

No comments:

Post a Comment