Na Peter Mwenda
RAIS Jakaya Kikwete na
mkewe Salma Kikwete jana waliongoza waombolezaji waliofika kuhani na kusaini
kitabu cha maombolezo nyumbani kwa marehemu Mbunge wa Jimbo la Mbinga
Magharibi, Kepteni John Komba aliyefariki juzi kwenye Hospitali ya TMJ, Dar es
Salaam.
Marehemu Komba ambaye
alifariki kwa shindikizo la Damu (BP) na Kisukari anatarajiwa kuagwa leo katika
viwanja vya Karimjee kuanzia saa 4 asubuhi na baadaye safari ya kwenda nyumbani
kwao Mbinga kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika Kesho kutwa.
Waziri Mkuu Mstaafu,
Edward Lowassa katika salamu za rambirambi alimtaja marehemu Komba kuwa alikuwa
mtu muhimu kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na watanzania wote kwa sababu alitumia
kipaji chake cha kuimba kuwaunganisha na kuwaburudisha.
Lowassa alisema kwa
upande wake, marehemu Kepteni Komba alikuwa mtu muhimu kwani alifanya kazi za
CCM kwa nguvu na moyo wake na kukifanya chama hicho kipoteze muhamasishaji
katika mambo mbalimbali ya jamii.
Naye Katibu Mkuu wa
CHADEMA, Willibroad Slaa alisema kifo cha Kepteni Komba ni cha watanzania wote
bila kujali chama kwa sababu marehemu alikuwa msanii mwenye kipaji cha hali ya
juu kuburudisha watanzania.
Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Dar es Salaam,Ramadhani Madabida
alisema CCM imepata pigo kubwa lakini kwa sababu kila mwanadamu aliandikiwa
siku ya kuzaliwa na kufa kwake hakuna budi kukubali matakwa ya Mungu kuwa
amemchukua anayempenda.
Marehemu Komba ambaye
alikuwa asafiri jana kwenda nchini Ethiopia katika Kamati ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto akiwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo imelezwa kuwa
kifo chake kimetokea ghafla.
Wengine waliofika
kuhani msiba wa Komba ni Spika wa Bunge, Anna Makinda ambaye alisema marehemu
alikuwa mchapa kazi na mwadilifu na hakuwa mtu wa majungu katika vikao vya
bunge na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hussein Mwinyi alisema marehemu alikuwa
akijitahidi kuhakikisha wananchi wa Jimbo lake wanapata huduma muhimu.
Naibu Waziri wa
Fedha, Mwingulu Mchemba, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), Hawa Ghasia, wabunge wa Chadema jimbo la Arumeru, Joshua Nasari,
Mbunge wa Arusha mjini, Godles Lema na waombolezaji wengine.
Msemaji wa Kampuni ya
TOT Plus, Gasper Tumaini alisema mwili wa marehemu Komba ulitarajiwa kuwasili
nyumbani kwake jana saa 11 jioni kwa ajili ya kuagwa na waombolezaji ambao
hawatapata nafasi kesho na baadhi ya
ndugu, jamaa na marafiki walitarajiwa kuondoka jana jioni.
Tumaini alisema
kutakuwa na mabasi sita yatakayochukua waombolezaji na magari mengine matatu
ambayo yatatangulia na mwili utafuata kesho kwa ndege baada ya heshima za
mwisho Karimjee.
mwisho
No comments:
Post a Comment