TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Thursday 24 July 2014

Mwaiposa aiomba serikali kuharakisha fedha za kukarabati madaraja Ukonga


Na Peter Mwenda

MBUNGE wa Jimbo la Ukonga, Eugine Mwaiposa ameiomba Serikali kutoa haraka fedha iliyoidhinisha sh. Bil. 3.9 kwa ajili kukarabati barabara za Jimbo la Ukonga ilizoharibiwa na mvua Aprili mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana alisema fedha hizo zinahitajika haraka ili kurudisha mawasiliano kati ya eneo moja kwenda jingine yaliyotenganishwa na mvua hizo na kusababisha kupanda kwa gharama za huduma za jamii kaama vyakula na usafiri.

Alisema Serikali katika awamu ya kwanza ya ukarabati huo ilitoa fedha kutoka mfuko wa maafa jumla ya Sh. bil. 1.5 zilizotumika kukarabati baadhi ya madaraja ambayo yalikatika karibu maeneo yote ya jimbo hilo.

Mbunge Mwaiposa alisema jimbo lake ni kati ya yale yaliyoharibiwa vibaya na mvua na mengi kukosa kabisa mawasiliano kama vile barabara ya Chanika na Msongola kupitia daraja la Mvuti, barabara ya Msongola kwenda Kivule na Kitunda kwenda Magole B kupitia daraja la mto Mzinga.

Alisema barabara nyingine ni kutoka Gonga la Mboto kwenda Ulongoni A na B ambapo madaraja mawili yalibomolewa na barabara itokayo Ukonga kwenda Mongo la Ndege kupitia daraja la Kinyerezi.

Mwaiposa alisema pamoja na fedha hizo kutolewa lakini bado zipo barabara na madaraja mengine ambayo hayajapata fedha kama vile barabara ya kutoka Kiltex kwenda Bangulo na Kitunda kwenda Mwanagati.

Alisema barabara nyingine ambazo hazikupata fedha lakini zimeombewa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ni kutoka Chanika kwenda Machimbo, Kivule kwenda mto Nyang'andu, Chanika Msumbiji kwenda Nzasa na Kibeberu kwenda Magole,

Alisema wakati wa uhakiki wa barabara zilizobomolewa na mvua zipo ambazo hazikutambuliwa kuharibika kwake ambazo ni barabara ya Dunda yenye mita 2,000, Pugu Mpakani mita 3,000, Barabara ya Mbondole Chanika na Yange Yange.

Mbunge huyo alisema pamoja na juhudi za Serikali kutenga mafungu bado tatizo la miundombinu ya barabara ni changamoto katika maeneo ya pembezoni ya Jiji la Dar es Salaam.

Alisema barabara hizo zilitengenezwa zitasaidia kupunguza msongamano wa magari mengi kukimbilia katika katika barabara kuu za jiji la Dar es Salaam.

Aliomba Serikali ifungue milango kwa watu na makampuni binafsi kuwekeza kwenye barabara na baadaye kutoza tozo kwa magari yanayotumia barabara hizo ili kuharakisha maendeleo.

mwisho


No comments:

Post a Comment