TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Saturday, 31 May 2014

NITATUMIA MSHAHARA WANGU WA BUNGE KUSOMESHA YATIMA KISARAWE-JAFO

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akimnadi Seleman Said Jafo wakati wa kampeni za uchaguzi.

KWA wabunge wengi wanaomaliza muda wao wa miaka mitano ya kuwatumikia wananchi wao baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopita, wakati muda ukizidi kuyoyoma, matumbo yao yako moto kwa hofu ya kutojua majaaliwa yao, kama watarejea tena mjengoni au la.
Mbunge wa Kisarawe mkoani Pwani, Seleman Said Jafo.
Lakini hata hivyo, wapo baadhi yao ambao baada ya kufanikiwa kwa kiwango kikubwa kukidhi matakwa ya wapigakura wao, hivi sasa hawana wasiwasi wa kutetea tena nafasi zao, kwani wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuondoa kero, sambamba na kutimiza ahadi mbalimbali walizoahidi.
Miongoni mwa wabunge hao ni Seleman Said Jafo wa Kisarawe mkoani Pwani, ambaye pamoja na kuwa hii ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni, lakini ametatua kero nyingi ambazo wananchi wa jimbo lake walikuwa nazo kwa kipindi kirefu kilichopita.
“Ninaweza kusema nimejitahidi kiasi cha asilimia 90 ya ahadi nilizoahidi kwa wapiga kura wangu nimetekeleza, wananchi wa Kisarawe ni mashahidi wa suala hili, nadhani nimetimiza wajibu wangu kama Mbunge,” alisema Jafo katika mahojiano maalum hivi karibuni.
Akizungumzia kuhusu sekta ya afya, mbunge huyo alisema wakati akiingia madarakani, aliikuta hospitali ya wilaya hiyo, iliyojengwa mwaka 1975, ikiwa chakavu kiasi kwamba hata chumba maalum cha kuhifadhia maiti kilishindwa kufanya kazi na kuwalazimu wananchi wake kupeleka maiti kuhifadhiwa katika Hospitali za Temeke na Amana.
Lakini kwa sasa hali imekuwa tofauti kwani imefanyiwa ukarabati mkubwa na sehemu zote muhimu, ikiwemo mochwari zimetengenezwa.
Alisema wakati akipata ubunge, wilaya yake ilikuwa na zahanati 14, lakini katika kipindi chake, amewaongoza wananchi wake kuongeza zingine nane.
Katika moja ya vituo hivyo vipya vya afya vilivyojengwa, kile kilichopo Kijiji cha Chole kiliivutia hata kamati mojawapo ya Bunge wakati ilipokitembelea na kusema kilikuwa ni kizuri na mfano wa kuigwa kwani ndani yake kina wodi maalum ya wazazi, kikiwa kimegharimu kiasi cha shilingi milioni 37.
Alilipongeza Shirika  la Plan International kwa kuwa karibu na wananchi katika sekta ya afya kwani lilinunua vitu vyote muhimu katika wodi ya wazazi.
Alisema shirika  hilo limesaidia Kituo cha Afya Masaki, Zahanati  ya Kijiji cha Kisanga, gari  la  kubebea wagonjwa Wilaya ya  Kisarawe, vitu vyote hivyo vikiwa na thamani ya shilingi 1.2 bilioni, achilia mbali mafunzo maalum ya kiafya kwa  watumishi wa vituo  hivyo.
Akielezea mafanikio zaidi katika sekta hiyo, alisema uhusiano wake mzuri na Kairuki Foundation, alipata msaada wa gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya Masaki kilichopo Kijiji cha Masangu.
Kuhusu maji, mbunge huyo mwenye umri wa miaka 41, alisema kero hiyo ilikuwa kubwa na iliwapa shida mno wananchi wa Kisarawe, lakini  kwa  jitihada zake amefanikisha  mradi mkubwa wa maji  wenye  thamani ya sh.mil. 540 ambao pia umefadhiliwa na Plan International  kwa  kushirikina  na serikali.
Aidha, kwa ushirikiano mzuri  na benki ya dunia, amefanikisha ujenzi wa visima katika vijiji tisa huku serikali ya China ikiwa katika ujenzi wa visima 30.
Plan International pia wamehusika katika mradi  mkubwa wa usambazaji maji mitaani katika Kijiji cha Gwata kwa kutumia chanzo cha mto Ruvu na wameweza kukamilisha  mradi mkubwa wa maji wenye  thamani ya shilingi milioni 375 uitwao Kuruyumatayo.
Katika miundombinu ya barabara, mbunge huyo alisema mkakati uliopo ni kuhakikisha kila mtaa unapitika na hivi sasa ujenzi unaendelea kuanzia Kisarawe mjini kwenda Maneramango na vijiji vya jirani.
“Udongo wa Kisarawe ni  mbaya sana hasa wakati wa mvua na ndiyo maana pia nguvu  nyingine nimeihamishia ili kupata  barabara yenye kiwango safi,” alisema na kusisitiza kuwa lengo ni kuwa na barabara za lami jimbo zima.
Kuhusu ulinzi na usalama, mbunge huyo alisema hiyo ni changamoto kubwa kwake, kwani kituo kikuu cha polisi jimboni kwake hakina ubora unaotakiwa.
“Rais Jakaya Kikwete alipofika hapa Oktoba mwaka jana, moja ya kilio nilichompa ni kituo cha polisi cha kisasa na nyumba za askari wake, alilichukua na linafanyiwa kazi,” alisema.
Juu ya upatikaji wa nishati ya umeme, mbunge huyo alisema wakati akiingia madarakani, ni vijiji vinne tu ndivyo vilivyokuwa na huduma hiyo muhimu, lakini katika kipindi chake, amepanua upatikanaji wa umeme hadi kufikia vijiji 26 kati ya 79 wilayani hapo.
Hadi kufikia 2015 anaamini vijiji vingi zaidi vitapata umeme.
Akilizungumzia Bunge Maalum la Katiba, alikerwa na kejeli, matusi na vijembe vinavyoendelea, kwani hilo siyo jambo walilotumwa na wananchi.

Alitaka sheria zitumike kuwabana wabunge wa namna  hiyo, ili mijadala ipate nafasi kubwa ya kufanyiwa kazi, huku akisisitiza kuwa muundo wa muungano wa serikali mbili ndiyo unaofaa na kuhitajiwa na watu wengi.
Amewaasa wajumbe wa bunge hilo kuzingatia kanuni ili kufikia matarajio ya utungwaji wa katiba mpya ambayo itawaongoza Watanzania kwa miaka mingi ijayo.
Alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa Kisarawe kumpa tena nafasi hiyo katika uchaguzi ujao ili aendelee kufanya mambo makubwa.

No comments:

Post a Comment