NCCR Mageuzi yapinga Bunge kutoneshwa 'live'
Na Peter Mwenda
CHAMA cha NCCR Mageuzi kimesikitishwa na taarifa ya Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilila kuzuia kurusha matangazo moja kwa moja kutoka bungeni badala yake kufanyiwa uhariri na kuchujwa kwanza kabla ya kuwafikia wananchi.
Kaimu Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Bw. Faustin Sungura akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, alisema chama chake kinapinga kwa nguvu zote hatua zozote zinazotaka kuchukuliwa na mamlaka yoyote kuzuia matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni.
"Tunapinga hatua hizo kwa sababu hoja na sababu za kutekeleza azma hiyo kama ilivyotolewa na Katibu wa Bunge ni hoja dhaifu na hasi" alisema Bw. Sungura.
Alisema vurugu zinazodaiwa kutokea bungeni haziwezi kukomeshwa kwa kuzuia kurusha matangazo ya moja kwa moja na kuongeza kuwa vurugu kama zipo zinaweza kukomeshwa kwa utaratibu wa kawaida kwa kutumia kanuni.
Bw. Sungura alisema kutumia kanuni hizo bunge linakuwa na mlalamikaji wa vurugu, mlalamikiwa anapewa nafasi ya kujitetea na uamuzi kutolewa na kusema kuwa matukio kama hayo yaliwahi kutokea bungeni kwa wabunge Augustine Mrema (Vunjo),Thomas Ngawaiya (Moshi Vijijini),Philemon Nderamburo (Moshi Mjini) Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) na John Mnyika (Ubungo)na kupewa adhabu.
Alisema kuzuia matangazo ya moja kwa moja kupitia luninga hakuwezi kumzuia mbunge anayejisikia kuongea kinachodhaniwa ni pumba asiongee, hakuzuii baadhi ya wabunge kutafakari kwa makini, kutumia muda mwingi kwenye simu zao za mikononi badala ya kuwawakilisha wananchi.
Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema mawazo ya Katibu wa Bunge hayalengi kuzuia vurugu bali yanalenga kuzuia watu walio nje ya bunge wasione vurugu na hiyo haina tofauti na mtu kuvaa nguo mpya juu ya mwili mchafu.
Alisema mawazo ya Katibu wa Bunge yanakinzana na ibara ya 18 (d) ya Katiba ya nchi inayosema kila mtu anayohaki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na jamii.
Bw. Sungura alisema NCCR Mageuzi inaamini kuwa matukio yote yanayotokea bungeni kama kufanya fujo, kulala usingizi bungeni, kujishughulisha na simu wakati wa bunge, kuongea hovyo bila utaratibu,Spika na Naibu wake kushindwa kuendesha bunge ni mambo muhimu ambayo wananchi wanapaswa kuyajua.
Alisema wananchi wakiyajua hayo wanapata fursa ya kufanya maamuzi katika kipindi kijacho cha uchaguzi kwa maana hiyo bunge halitakiwi kunong'ona bali lisikike kwa ukamilifu.
Alisema pia NCCR inapinga bunge kuchukua hatua ya watu waliomwandikia ujumbe mfupi na kuwapigia simu za mkononi Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda na Naibu wake Bw. Job Ndugai kwa vile ni simu zao binafsi hazijasajiliwa kwa ajili ya bunge.
mwisho
No comments:
Post a Comment