Njaa yapiga hodi Kondoa
Na Massare Damiani,Kondoa.
SHULE za msingi katika kata ya Hondomairo
tarafa ya Kolo wilayani Kondoa huenda zikafungwa wakati wowote kutokana
na kukosa chakula unaosababisha njaa kali ambapo
wananchi sasa wanafikiria kuhama makazi yao kwenda maeneo mengine kuhemea chakula.
Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Hondomairo, Bw.
Kirangi Shaabani Hussein wakati akiwa njiani kuelekea ofisi za
halmashauri ya wilaya ya Kondoa kushughulikia tatizo hilo,alisema kuwa
hali katika kata yake ni mbaya na kinachosikitisha zaidi ni kata yake
kutokuwepo kwenye orodha ya mgao wa chakula tani 50 zilizotoloewa na
serikali kuu.
Diwani Kirangi amelalamika kuwa kutokana na hali
ngumu ya maisha hivi sasa katika kata yake wananchi kukosa chakula, hata
shughuli za maendeleo zimekwama na wananchi wanashindwa kufanya
kazi zao za mashambani
kutokana na ulegevu walio nao.
"Nimekuwa nikitoa taarifa tangu
mwaka jana Juni na serikali na halmashauri wamekuwa wakinisikia na
kuahidi kushughulikia tatizo hilo,sasa inakuwaje leo kata yangu inakuwa
haipo kwenye orodha ya mgawo wa chakula?amehoji diwani Kirangi kwa
uchungu.
Alisema kuwa yeye mwenyewe amelazimika kutoa chakula
alichokuwa nacho ndani ya nyumba yake magunia 10 na kuwagawia wananchi
akidhani kuwa atawasogeza hadi katika mgao wa chakula cha serikali
lakini kumbe hakuna cha serikali na yeye mwenyewe amebakia hana chakula
cha kuikimu familia yake.
"Mimi nashangaa kama serikali kweli
itaamua kutowajali watu wa kata yangu ya Hondomairo ambao nao ni
wanaKondoa waliokumbwa na tatizo la njaa,au kama serikali inapuuza kwa
kudhani kuwa ni mzaha,basi ngoja watu wafe na atakayejibu sijui ni
nani,"amesisitiza.
Kata hiyo ya Hondomairo na vijiji vya Mwembeni
chenye watu 3494,Hondomairo watu 2896,na Mtiryangwi watu 3696
jumla ni watu 10,086 na kaya ni 2224 ambazo licha ya ukosefu wa chakula
lakini pia lipo tatizo kubwa la maji kwa wananchi kutembea umbali mrefu
kutafuta maji.
Diwani Kirangi ameiomba serikali kufanya haraka
kwani bila kuwanusuru wananchi hao kwa chakula cha msaada hakuna lolote
litakalofanyika la maendeleo na wananchi hata mazao waliyolima
mashambani mwao hawataweza kuyahudumia ipasavyo hivyo kupata hasara ya
nguvu zao,mbegu na fedha za kulimia.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment