KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Harry Kitilya pichani,
amesema kuwa kitendo cha wananchi kuficha fedha katika mabenki ya nje
kinaikosesha serikali mapato.
Akizungumza katika semina ya waandishi wa habari juu ya uelewa wa
vitendo vya udanganyifu vinavyofanyika nchini, Kitilya alisema kuwa
iwapo fedha hizo zingeweza kuhifadhiwa nchini serikali ingeweza
kukusanya kodi kupitia fedha hizo.
Mbali na hilo, Kitilya alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa vitendo vya
udanganyifu hadi sasa taifa linapoteza asilimia 5 ya pato la taifa kila
mwaka.
Kamishna huyo alisema kuwa kiasi cha dola trilioni 3.5 kilipotea
duniani kwa njia ya udanganyifu katika kipindi cha mwaka jana kutokana
na shughuli mbalimbali kufanywa kwa mitandao.
“Jambo hilo ni janga kwa taifa kwa kuwa linafanyika katika maeneo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na uhasibu, ununuzi, uuzwaji na hata katika
eneo la ukusanyaji kodi, huko ndiko kumekuwa na tatizo kubwa,” alisema.
Kitilya aliongeza kuwa ndani ya mamlaka hiyo wamekuwa wakipata
matatizo makubwa hasa katika uingizaji wa magari na leseni, kwani wezi
hao wamekuwa wakiandaa nyaraka bandia ambazo zinakuwa na mihuri ya
mamlaka hiyo.
Alitaja maeneo mengine kuwa ni pamoja na taasisi za kifedha, zikiwemo
benki ambapo wezi wanaweza kuingiza nyaraka bandia na kuchukua fedha
pasipo wahusika kubaini.
Kitilya aliitaka jamii kuwa makini na kutosita kutoa taarifa ili
wahusika hao waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Nyinyi waandishi mna kazi kubwa katika hilo, ni muhimu mkikutana na
vitendo hivyo mkaviweka wazi ili viweze kujulikana na kuzuiwa
visijitokeze,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Chapter, Lusekelo Mwaseba, alisema
kuwa hadi sasa ripoti mbalimbali zimefanyika duniani ili kubaini ukubwa
wa tatizo hilo ambapo kwa hapa nchini makampuni matano yalifanyiwa
utafiti katika kipindi cha mwaka 2011.
Alisema kwa sasa wanashughulikia eneo la afya ambapo kuna udanyanyifu
unaofanywa na baadhi ya watu wakitumia huduma za kiafya pasipo kuwa
wanachama halali.Tanzania Daima.

No comments:
Post a Comment