Beki wa Yanga, Stephano Mwasika akimiliki mpira huku akizongwa na beki
wa Simba, Nassoro Masoud 'Cholo' katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka
Tanzania Bara unaoendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam
Kaseja atika harakati za kukomboa.
YANGA imetoka sare ya kufungana bao 1-1 na wapinzani wao
wa jadi, Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliopigwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuanzia saa 1:02 usiku.
Yanga ambao walimaliza mechi hiyo wakiwa pungufu baada ya
Simon Msuva kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu Juma
Nyosso, ndio waliohaha kusawazisha bao, baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema
la kiungo Amri Kiemba.
Hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0,
lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba dakika ya pili.
Katika kubahatisha huko, Mbuyu Twite alifumua shuti zuri
dakika ya 38 kutoka wingi ya kulia, ambalo lilitoka nje sentimita chache.
Katika dakika ya 63, beki Paul Ngalema aliunawa mpira katika
harakati za kuokoa na refa Mathew Akrama akaamuru penalti, ambayo ilikwamisha
kimiani kiufundi na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Katika dakika ya 77 Mathew Amkrama alimtoa nje kwa kadi
nyekundu ya moja kwa moja Simon Msuva, baada ya kumkita Juma Nyosso,
aliyemkanyaga ‘kwa bahati mbaya’. Msuva alichezewa rafu na Nyosso na tayari
refa alikwishapuliza filimbi na kumpa kadi ya njano beki huyo wa Simba, lakini
kiungo huyo wa Yanga akaponzwa na hasira za kitoto.
Pamoja na Yanga kubaki pungufu, waliendelea kucheza vema na
mashambulizi yalikuwa ya pande zote mbili. Refa Akrama alishindwa kuumudu
mchezo na maamuzi yake mengi yalikuwa chungu kwa Yanga, mfano Haruna Moshi ‘Boban’
alipomchezea rafu mbaya beki Kevin Yondan hadi akashindwa kuendelea na mchezo,
na nafasi yake ikachukuliwa na Juma Abdul alimpoza kwa kadi ya njano.
Hakumchukulia hatua yoyote kipa Juma Kaseja aliyeonekana
kupoteza muda tangu mwanzo, na alimpa onyo tu zaidi ya mara tatu.
Alipingia Abdul alikwenda kucheza beki ya kulia na Mbuyu
Twite akahamia katikati kucheza na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 13, ndani ya mechi
tano na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, wakati Yanga imefikisha pointi nane na
kubaki nafasi ya tano, kwani Coastal Union imetoa sare ya 2-2 na JKT Oljoro
mjini Arusha na kufikisha pointi tisa.
No comments:
Post a Comment