TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Saturday, 15 September 2012

Dkt. Migiro amwagia sifa Rais Kikwete

Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete amesifiwa kuwa kiongozi wa kwanza Tanzania kuweka dira ya wanawake kushika nyadhifa za uongozi katika ngazi mbalimbali za kitaifa.

Hayo yalisemwa jana na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Dkt. Asha-Rose Migiro alipozungumza na wanawake katika sherehe aliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ya kumpongeza na kumkaribisha nyumbani.

Dkt. Rose alisema takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha uongozi wa awamu ya Nne ya Rais Kikwete wanawake wameshika nyadhifa mbalimbali kuanzia ngazi ya chini hadi za juu.

"Mafanikio ya kuwezesha wanawake amefanikiwa kwa kuweka tofali katika msingi uliowekwa na marais waliopita" alisema Dkt. Migiro.

Alisema nafasi aliyoipata ya kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha anasimamia maendeleo, usalama,amani na uhai wa binadamu.

Dkt. Migiro alisema alifanikiwa kusimamia mambo hayo kutokana na Tanzania kumlea katika misingi hiyo na kuilinda ipasavyo.

Alisema Katibu Mkuu wa UN, Ban Kin-Moon ameipa heshima Tanzania kwa kumchangua kushika wadhifa huo kwa kuwa alikuwa anaiamini kutokana na sifa ilizokuwa nazo za amani duniani.

Alisema ili wanawake wapate mafanikio zaidi nchini lazima wadumishe umoja, mshikamano katika kushughulikia maendeleo yao na watoto.

Naye Mke wa Rais Kikwete, Mama Salma Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo alisema mafanikio aliyoyapata Dkt. Migiro ni ya watanzania wote hivyo hakuna budi kujivunia na kufurahia kwani ameitangaza na kuijengea heshima.

Alisema Dkt. Migiro akiwa Umoja wa Mataifa alifanikiwa kusimamia uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia katika kupiga vita vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Mama Kikwete alisema Dkt. Migiro wakati akiwa na wadhifa huo kila alipopata fursa alihimiza mamlaka katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutunga sera na sheria zinazozingatia haki za wanawake na usawa wa kijinsia na kuomba wanawake wapewe fursa kushika nafasi za uongozi katika jamii.

"Juhudi zake na wenzake duniani ndizo zilizosababisha kuanzisha kwa idara inayoshughulikia masuala ya wanawake na usawa wa kijinsia kwa umakini na ufanisi (UN Woman) ambayo matunda yake yamekwisha anza kuonekana" alisema Mama Kikwete.

Katibu Mkuu wa UWT, Bi. Amina Makilage akisoma risala ya umoja huo alisema Dkt. Migiro ni mwanamke wa kwanza Afrika kushika nafasi hiyo tangu umoja huo ulipoanzishwa miaka 67 iliyopita.

Alisema katika uongozi wake alijitahidi kupaza sauti ya mwanamke na msichana katika ngazi ya kimataifa katika kupinga vitendo vya kikatili na kuhakikisha mwanamke anapewa fursa katika uongozi.

Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na wake wa marais wa awamu ya Kwanza Mama Maria Nyerere, Mama Sitti Mwinyi na viongozi mbalimbali waliowahi kushika nyadhifa serikalini, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Said Mecky Sadick naye alihudhuria.

mwisho












No comments:

Post a Comment