*Yailaza Botswana
32-23, yatwaa ubingwa wa pili
MKE wa Waziri
Mkuu, Mama Tunu Pinda ametimiza ahadi aliyoitoa kwa timu ya Taifa ya Netiboli (Taifa
Queens) ya kuwapa sh. milioni moja kila mchezaji endapo wangetwaa ubingwa
wa Kombe la Mashindano ya Afrika ambayo yamemalizika jana jijini Dar es Salaam.
Mama Pinda ambaye ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kuisaidia Taifa Queens Ishinde, alitimiza
ahadi hiyo jana usiku (Jumamosi, Mei 12, 2012) katika hafla fupi ya kuwakabidhi
wachezaji hao bankers’ cheques zao.
Wachezaji 16 walipatiwa sh. milioni moja kila mmoja, na maafisa sita wa timu
walipewa sh. 800,000 kila mmoja. Jumla ni sh. milioni 20.8/-
Akizungumza
na wachezaji hao, viongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), na baadhi
ya Wake wa Viongozi ambao ni wanachama wa New Millenium Women Group, Mama Pinda
aliwapongeza wachezaji hao kwa jinsi walivyojituma na kufanikiwa kushinda
nafasi ya pili.
Alisema
vijana hao wamejituma na kufanikiwa kuifunga timu ngumu ya Botswana ambayo
kimataifa ina hadhi kubwa kuliko Taifa Queens na kwamba juhudi zao zimeweza kuipandisha
hadhi Tanzania katika ulimwengu wa michezo. Aliwatakia ushindi zaidi katika
michuano hiyo ambayo mwakani imepangwa kufanyika nchini Malawi.
Aliwashukuru
Watanzania wote na taasisi ambazo zilijitolea kwa hali na mali kuhakikisha kuwa
timu hiyo inafanya vizuri tangu ikiwa kambini hadi wakati wa mashindano.
Akitoa
shukrani kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha wa timu hiyo, Lilian Sylidion,
alisema ahadi ya Mama Tunu Pinda ambayo aliitoa wakati wa ufunguzi wa
mashindano hayo, Mei 8, mwaka huu iliwapa hamasa na kuchochea kupatikana kwa
ushindi huo.
“Kwa kweli
ile ahadi ya kitita cha shilingi milioni moja ilitufanya tuwe na ari zaidi...
kama timu tulidhamiria kuchukua kombe. Mimi binafsi nilisema hata kama ni
kuvunjika mguu acha wanivunje lakini nihakikishe siikosi hiyo one m,” alisema huku akishangiliwa na
wenzake.
Kombe hilo
limechukuliwa na Malawi ambao walikuwa ni mabingwa watetezi, Taifa Queens
imeibuka washindi wa pili na washindi wa tatu ni Zambia. Malawi wamemaliza
mashindano wakiwa na pointi 10 kwa kushinda mechi zote tano wakifuatiwa na
Taifa Queens ambayo imepata pointi nane baada ya kushinda mechi nne na kupoteza
mechi moja ilipofungwa na Malawi. Zambia imepata pointi sita, Botswana pointi
nne, Zimbabwe pointi mbili na Lesotho haikuambulia kitu.
Hadi kupata
ushindi huo, (Mei 8, 2012) Taifa Queens iliicharaza Lesotho mabao 57 -13, (Mei
9, 2012) Taifa Queens ikafungwa na Malawi 34-30; (Mei 10, 2012) Taifa Queens
ikailaza Zambia 37-33; (Mei 11, 2012) Taifa Queens ikaicharaza Zimbabwe 46-15;
na jana (Mei 12, 2012) Taifa Queens ikailaza Botswana 32-23.
Baadhi ya
wake wa viongozi waliohudhuria mechi hiyo pamoja na Mama Tunu Pinda ni Mke wa
Makamu wa Rais, Bi. Asha Bilal ambaye alikuwa mgeni rasmi, Mama Hasina Kawawa, Mama
Germina Lukuvi, Mama Pamela Matayo, Mama Sophia Mukama, Mama Janet Magufuli, Mama
Nahodha, Mama Mwakyembe na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya
kuisaidia Taifa Queens ishinde.

No comments:
Post a Comment