TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Tuesday, 8 May 2012

TIMU ya Taifa ya Netiboli (Taifa Queens) ifunga timu ya Taifa ya Lesotho kwa mabao 57-13.






TIMU ya Taifa ya Netiboli (Taifa Queens) imeanza vema pazia la michuano ya Kombe la Afrika kwa mchezo huo baada ya kuifunga timu ya Taifa ya Lesotho kwa mabao 57-13.

Mchezo huo wa ufunguzi ulifanyika katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Fenela Mukandala, Mke wa Waziri Mkuu Tunu Pinda pamoja na wake wa  Makamu wa Rais mama Asha Bilali na wake wa Mawaziri, Mabalozi na viongozi mbalimbali.

Katika mchezo huo kikosi cha Taifa Queens kilionekana kuimarika zaidi mwanzo hadi mwisho wa mchezo huku wachezaji machachari wa Lesotho wakishindwa kuhimili mikikimikiki ya Taifa Queens.

Katika kota ya kwanza ya mchezo huo Taifa Queens iliongoza kwa mabao 13-3, kota ya pili ikaongoza kwa mabao 23-9 yaliyoiwezesha Taifa Queens kwenda mapunziko ikiwa kifua mbele.

Taifa Queens iliokuwa ikiongozwa vema na mfungaji wake wa kutegemewa Mwanaidi Hasan ambaye pia ni mwanamichezo bora wa tuzo za Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) mwaka jana, aliyeibuka na gari iliingia kipindi cha pili cha mchezo huo kwa kufanya mabadilio kwa kumuingiza mfungaji Pili Peter na kumtoa Mwanaidi.

Katika kota ya tatu Taifa Queens iliendelea kuwapigisha jaramba wachezaji wa Lesotho kwa kuwafunga mabao 40-13 ambapo kota ya mwisho ikaichapa 57 huku Lesotho ikishindwa kufunga hata bao moja ambapo hadi mwisho wa mchezo Taifa Queens ikaibuka kidedea na ushindi huo mkubwa wa mabao 57-13.

Kabla ya mchezo huo Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya michuano hiyo Mama Tunu Pinda aliahidi kuwapa wachezaji hao sh. milioni moja kila mmoja endapo watahakikisha kombe la Afrika linabaki nyumbani.

Alisema kutokana na lengo la uchagishwaji fedha kwa ajili ya michuano hiyo kuvuka malengo waliyoyaweka fedha zote zitakazobaki mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo watakabidhiwa wachezaji.

Naye Mama Salma Kikwete amewashukuru wadau wote waliofanikisha kufanyika kwa michuano hiyo mikubwa na kukipongeza Chama Cha netiboli Tanzania (CHANETA) Kwa kuandaa mashindano hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yataitangaza nchi katika medani ya kimataifa.

Kwa upande wake Waziri wa Habari Vijana, Utamaduni na Michezo Fenela Mukandala ametoa rai kwa CHANETA na vyama vyote vya michezo kuhakikisha vinapanga programu zao vizuri zitakazoweza kuleta maendeleo na tija katika michezo.

Pia amelitaka Baraza la Michezo Taifa (BMT) kusimamia vema utekelezaji wake ili vyama vya michezo vilio chini yao visihahe katika dakika za mwisho mara zinapoandaa mashindano makubwa kama yaliyoweza kuandaliwa na CHANETA.


Michuano hiyo pia imehudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Netiboli Afrika Tebogo Lebotse na Mwakilishi kutoka Shirikisho la Netiboli Duniani (IFNA) Joan Smit.

Mchuano hiyo ya kombe la Afrika itaendelea kesho kwa michezo kati ya Malawi na Zambia, Botswana na Uganda, Zimbabwe na Lesotho, Tanzania na Malawi na mchezo wa mwisho utakuwa kati ya Uganda na Zimbabwe.

No comments:

Post a Comment