Peter Mwenda
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kitendo cha Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda kushindwa kuwachukulia hatua mawaziri saba wanaoshinikizwa kujiuzulu kunatokana na ulegevu wa Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari kama Rais Kikwete angekuwa amempa Waziri Mkuu nyenzo za kufanyika kazi tayari mawaziri hao wangekuwa wamefukuzwa kazi.
"Sasa kilichobaki ni chama chetu kushirikiana na vyama vingine vya upinzani kushirikiana ili kumshinikiza rais kuwa mtoa maamuzi"alisema Profesa Lipumba.
Alisema kitendo cha Waziri Mkuu Pinda kushindwa kutoa maamuzi kama kiongozi wa nchi kunaonesha dhahiri hana nyenzo za kufanyia kazi ndiyo maana mawaziri wanaotuhumiwa wameshindwa kuondolewa madarakani.
Profesa Lipumba alisema serikali imekuwa ombaomba, wananchi wake wanaishi maisha duni na bei ya vyakula iko juu kiasi cha kushindwa kumudu kununua chakula.
Alisema uongozi wa Rais Kikwete unatia wasiwasi katika miaka iliyobaki kabla ya kumaliza muda wake wa uongozi kuwa wananchi wanaishi maisha ya taabu.
Profesa Lipumba alisema kuibuliwa kwa mjadala wa maziri umetokana na kazi nzuri iliyofanywa na mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hivyo CUF inampongeza na inandaa utaratibu wa kushinikiza viongozi hao wawajibike.
Alisema CUF inandaa maandamano makubwa ya kutaka watu wote waliochukua fedha za serikali wachukuliwe hatua za kisheria.
Mwenyekiti huyo alisema nchi imekuwa ikididimia kiuchumi siku hadi siku huku Rais akishindwa kuchukua maamuzi wa kuadabisha baadhi ya watu wanaofuja mali za wananchi.
"Mfano ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw.David Jairo ambaye alikuwa awajibishwe Waziri Mkuu akasema Rais atachukua hatua akirudi safari lakini aliporudi alimrudisha madarakani" alisema Profesa Lipumba.
Alisema mawaziri na naibu wao hawaelewani na kila mmoja anafanya kazi kama apendavyo lakini Rais anayaona hayo lakini bado yuko kimya.
Profesa Lipumba alisema kutokana na hali hiyo inayonyamizwa kimya na Rais imekuwa ikisababisha mawaziri wengi kwenda kinyume na maadili ya kazi zao.
Alimpongeza mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe kwa kuanzisha mjadala wa kutokuwa na imani na Waziri Mkuu na kuongeza kuwa CUF inaunga mkono mjadala huo na kuwataka wabunge wake kuweka saini.
Alisema kwa kuwa bunge linamshunghulikia Waziri Mkuu Pinda, hivyo CUF kushirikiana na vyama vingine vya upinzani vimshughulikie Rais ili aweze kuwaondoa madarakani mawaziri wanaotuhumiwa.
mwisho
No comments:
Post a Comment