TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Friday, 6 April 2012

Bodi ya Utalii imechangia uchumi-Maige

Na Peter Mwenda
WIZARA ya Maliasili na Utalii imesema Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imeitangaza Tanzania kama moja ya nchi zenye vivutio vikubwa na vya pekee barani Afrika na duniani kwa ujumla na kuongeza idadi ya watalii kutoka kutoka 230,166 mwaka 1993 kufikia 867,994 mwaka 2011.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Bw. Maige alisema tangu kuundwa kwa Bodi ya Utalii  miaka 18 iliyopita, imechangia kuleta mafanikio katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini na kuleta ongezeko la mapato ya utalii kutoka dola za kimarekani milioni 146.84 mwaka 1993, hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 1.3 mwaka 2010.

"Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kuhudumia sekta ya Utalii ikiwa ni pamoja na kujenga miundo mbinu, kuongeza bajeti ya utangazaji, kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji, kuboresha huduma kwa watalii kama vile malazi, chakula na usafiri"alisema Bw. Maige.

Alisema ubora wa huduma kwa watalii sambamba na kuimarika kwa utangazaji wa utalii ndani na nje ya nchi ni masuala muhimu katika kuvutia watalii wengi zaidi kuja hapa nchini.

Waziri Maige alisema Serikali iko katika hatua za awali za kuiunda upya Bodi ya Utalii Tanzania ili kuifanya Mamlaka ya Utalii Tanzania ambapo pamoja na jukumu lake kuu la utangazaji utalii, itawajibika kudhibiti huduma na kusimamia shughuli zinazohusiana na utalii, ikiwa ni pamoja na kusajili kampuni za kitalii.

"Serikali inalenga kukiboresha chombo hiki, kukiimarisha na kukipa nguvu  zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake, nakupongeza Balozi Charles Sanga kwa kuteuliwa kwako na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania ambacho ni chombo muhimu sana  katika maendeleo ya sekta ya utalii hapa nchini"a lisema Bw. Maige.


Alisema jukumu la Bodi hiyo ni kuidhinisha mikakati na mipango ya muda mfupi na mrefu ya kutangaza utalii na kuona inatekelezwa ipasavyo, bajeti za Bodi ya Utalii na kushauri Wizara, Serikali kuhusu mbinu za kuboresha bajeti ya utangazaji utalii na kuishauri serikali juu ya mipango ya kukuza utalii na kuona jinsi Bodi ya Utalii inavyoweza kutoa mchango wake.

Waziri Maige alisema lengo la Wizara yake ni kufikia watalii mil. 1 mwishoni mwa 2013 na kuhakikisha utalii unaendelea kukua kwa  asilimia 8-10 kwa mwaka na hivyo kufikia walau watalii milioni 1.2 ifikapo 2015.

mwisho

No comments:

Post a Comment