Na Peter Mwenda
CHAMA Cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi (Albino) Wilaya ya Kinondoni kimegawa msaada wa nguo, kofia na Losheni vilivyotolewa na Shirika la Kikristo la Huduma za Wakimbizi (TCRS).
Akikabidhi nguo hizo Diwani wa Kata ya Ndughumbi aliyewakisilishwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Makanya Bw. Selemani Mweijeka alisema walemavu wa ngozi wasitishike na maneno yanayosemwa mitaani kutokana na hali yao ya ngozi.
Alisema albino wanastahili kupata huduma kama wengine na kuwataka wasikate tamaa kuwapeleka watoto wao shuleni kwani wana akili kama wengine.
Katika risala ya Albino hao iliyosomwa na Mweka hazina wao Bi. Mwamvua Kambi ilisema kuwa wanakabiliwa na changamoto za kukabiliwa na wagonjwa wengi wa saratani ya ngozi ambao wanahitajika kwenda kutibiwa KCMC,Kilimanjaro kukosa wafadhili wa kuaminika na kukosa vitendea kazi vya kisasa na samani za ofisi ya wilaya.
"Angalieni namna ya kutusaidia kwa sababu vyama vya walemavu havina mafungu maalum tunayopata kutoka Serikalini kutekeleza majukumu yake"alisema.
Pia katika risala hiyo albino hao waliomba Kamati ya Kata iwaingize katika mipango ya Maendeleo wasaidiwe kupata eneo la kujenga ofisi eneo la Mabwe Pande ili shughuli zao zifadhiliwe kupitia ruzuku kutoka Manispaa ya Kinondoni.
Mwenyekiti wa albino Kinondoni, Bw. Mussa Geuza alisema kuna ongezeko kubwa la walemavu wa ngozi katika wilaya hiyo na wengi wao wamepata mwamko wa kupeleka watoto wao shuleni.
Bw. Geuza alisema mwaka 2006 wilaya ya Kinondoni ilikuwa na wanachama albino 130 lakini wamejitokeza na kufia idadi yao 300 kati ya hao watoto ni 120 na watu wazima 180.
Alisema albino hao wanakabiliwa na huduma za mafuta ya kulainishia ngozi (losheni) ambazo kwa sasa zinauzwa ghali kulinganisha na uwezo wao hivyo wengi wao kushindwa kumudu kununua kunakosababisha kubabuka ngozi.
Mwenyekiti huyo alisema chama hicho wilaya ya Kinondoni kinajitahidi kuwa karibu na albino hao ili kutafutia ufadhili pale wanapozidiwa na magonjwa yanayosababishwa na ulemavu huo.
mwisho
No comments:
Post a Comment