Na Peter Mwenda
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)imekuwa ikikusanya fedha kutoka Kampuni za simu nchini na kuzitumia vibaya bila kufuata utaratibu wa kuomba kibali kutoka Wizara ya Fedha.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC)walibaini hayo jana wakati wakipitia mahesabu ya TCRA ya mwaka 2010/2011 na kukuta kuwa kuna matumizi mabaya kwani katika mafunzo ya wafanyakazi watatu pekee imegharimu sh. bil. 2.3.
Kamati hiyo pia imeagiza TCRA kuacha kulipa wajumbe wa Bodi fedha nyingi pia kuacha kulipa kutumia dola badala ya kutumia fedha za Tanzania.
Mwenyekiti wa Kamati ya POAC, Bw. Deo Filikunjombe alisema wamekataa mahesabu ya TCRA kutaka wapitia upya mahesabu hayo na kurekebisha kasoro zote zilizopo na kujieleza sababu za matumizi mabaya ya fedha za umma.
Bw. Filikunjombe alisema Kamati inashangaa kuona gharama za ujenzi wa jengo la Mawasiliano Tower zipande kutoka Bil. 27.4 ambazo zilikuwa zitumike zipande hadi kufikia Bil. 45 wakati kulikuwa na mshauri aliyelipwa fedha kufanya makadirio ya ujenzi.
Mjumbe wa Kamati hiyo Bw. Murtaza Mangungu alihoji kuwa inakuwaje makampuni yaliyoneshwa kwenye kumbukumbu kuwa yanalipa kodi ni matano wakati ni kampuni saba za simu zinazolipa kodi.
"Mnakusanya fedha bila kujua kazi ya kuzifanyia, mnamwajiri Mhasibu kwa ajili ya kuandika mahesabu yenu lakini pia mnamlipa mshauri wa mahesabu ambaye mnalipa fedha nyingi,punguzeni matumizi, simamisheni wajumbe wa bodi kulipa fedha za kigeni"
"Mmelipwa dola mil. 600 kutoka Vodacom, pia Zantel imewalipa dola mil.1.6 lakini hazikuwekwa kwenye hesabu zetu, tumegundua kuwa mashirika mengi ambayo yanapata fedha bila kuvuja jasho wanatumia fedha hizo vibaya" alisema Kaimu Mwenyekiti POAC.
Alisema kutokana na kasoro hizo wamekataa mahesabu ya TCRA na kumtaka Mwenyekiti wa Bodi Jaji Mstaafu, Buxton Chipeta kukaa na Menejimenti kurekebisha mahesabu hayo.
Bw.Filikunjombe alisema TCRA ambayo walisema inawajibika kwa Waziri wa wizara husika lakini matumizi yao lazima yapitishwe na Wizara ya Fedha ndipo itumie fedha hizo.
Alisema matumizi mabaya ya TCRA yananyima nafasi ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu kupata mikopo kwa ajili ya masomo yao kutokana na fedha nyingi kutumika kutoa tenda kwa upendeleo na gharama za chini lakini zinapanda kutokana na kufichwa kwa tenda na kuchangia kushuka kwa uchumi wa nchi.
Mbunge wa Viti Maalum Tanga, Bi. Amina Mwidau alisema TCRA imefanya wizi wa waziwazi katika mahesabu hayo na kuutaka manejimenti kufanya mabadiliko katika utendaji wao ili kuokoa uchumi wa Tanzania.
mwisho
No comments:
Post a Comment