Na Peter Mwenda
MAMIA ya waombolezaji jana walifurika kuaga mwili wa Mwenyekiti wa zamani wa Bodi ya Benki ya Akiba (ACB), Bw. David Mosha aliyefariki dunia Jumatatu Oktoba 10 eneo la Kabuku, Tanga.
Waombolezaji hao wakiwa na nyuso za huzuni walipita mbele ya jeneza lililokuwa na mwili wa marehemu Mosha nyumbani kwake Mbezi Beach kabla ya kupelekwa kanisani na baadaye kuanza safari ya kwenda kwenye mazishi nyumbani kwao Kilema Mkyashi, mkoani Kilimanjaro.
Msemaji wa familia Bw. Salutary Mosha ambaye ni mdogo wa marehemu alisema kifo cha kaka yake kimeacha pengo kubwa kwa familia na watanzania waliowahi kufanya naye kazi wakati wa uhai wake.
"Marehemu alikuwa mchapa kazi na hajawahi kwenda likizo katika maisha yake,likizo kwake ilikuwa usingizi, alisaidia watu wengi, alikuwa akitoka shambani kwake Gomba alikuwa akamalizie ujenzi wa holi (jumba la Mikutano) katika shule ya msingi Mkyashi, Kilema Moshi.
Alisema marehemu kaka yake alifariki Jumatatu iliyopita (Oktoba 10) saa 5.20 akiwa katika gari aina ya Toyota Double Cabin namba T592 AAM lilikuwa likiendeshwa na dereva Justine Temu kuacha njia na kugonga mti.
Msemaji huyo alisema katika ajali hiyo marehemu alifariki papo hapo na mwili wake kuhifadhiwa katika hospitali ya Korogwe.
Wakati wa uhai wake marehemu Mosha alifanya kazi katika taasisi mbalimbali kama vile SIDO na kuwa mmoja wa waanzilishi wa Kampuni ya Inter Consult na pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Gomba Industry Ltd ya Tanga.
Marehemu ameacha mke na watoto saba, Mungu ilaze roho ya marehemu mahali pema Peponi Amina.
mwisho
No comments:
Post a Comment