TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Wednesday, 26 October 2011

Kamati ya Zitto Kabwe yabaini madudu VETA

*Fedha za umma zapitia akaunti binafsi
*Yamuweka kiti moto mkurugenzi wake
 Peter Mwenda na Salim Nyomolelo

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), ambaye Mwenyekiti wake ni Bw. Zitto Kabwe, imeshindwa kupitisha hesabu ya Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), baada ya  kugubikwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu, hivyo kuzuia hofu ya kuwepo kwa aina fulani ya ufisadi.

Kamati hiyo ilikataa mahesabu ya VETA baada ya kubaini kuwa fedha za mamlaka hiyo kupitia kwenye akaunti za watu binafsi, kabla ya kusambazwa kwenye vyuo vya mamlaka hiyo nchini.

Akizungumza kwenye kikao cha kamati hiyo Dar es Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa POAC Bw.Murtaza Mangungu, alisema kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa mbele ya kamati yake, VETA ilikuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma tangu mwaka 2008.

Alisema mhasibu wa VETA alikuwa na tabia ya kuweka fedha hizo kwenye akaunti yake binafsi, kabla ya kuzituma kwenda vyuo husika jambo ambalo ni kinyume na sheria,taratibu na Kanuni.

Wajumbe wa kamati hiyo walionesha kukasirishwa na hali hiyo, huku baadhi ya wabunge wakihoji kuwa mamkala hiyo iliwahi kupata hati chafu ya ukaguzi, lakini bado haijajirekebisha na kutaka hatua zaidi zichukuliwe.

Pia kamati hiyo, ilihoji sababu za VETA kuwasilisha taarifa yake kwao siku moja kabla ya kikao cha kamati, badala ya kufanya hivyo siku tano kabla, kama ilivyofanyika kwa mashirika mengine.

Kamati hiyo ilisema kitendo hicho ni dharau kwa kamati.

Kamati hiyo ilisema VETA imekuwa na tabia isiyoridhisha katika matumizi yake na kuongeza kuwa hata fedha za ruzuku ya matumizi ya kawaida hupitishwa kwenye akauti za watu binafsi, badala ya taasisi hiyo kama inavyotakiwa.

Kamati hiyo pia ilihoji sababu za mamlaka hiyo, inayotegemewa kufanya kazi kwa muda wa miezi saba bila kuwa na bodi jambo ambalo ni hatari na linaweza kusababisha mianya ya matumizi mabaya ya fedha za Umma.

"Mmefanyaje kazi kwa muda wa miezi saba bila ya kuwa na bodi kwa nini?"Alihoji Bw. Mangungu.

Mahojiano kati ya VETA na kamati ya Bunge

Mahojiano kati ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mkurugenzi wa VETA Bw. Zebediah Moshi, ilikuwa kama ifuatavyo;

Kaimu Mwenyekiti wa kamati: Ni wapi Mkurugenzi ulikuwa ukipata ushauri?

Mkurugenzi wa VETA: Niliwasiliana na wizara moja kwa moja.

Kaimu Mwenyekiti:  Unajua Bodi inawajika kwa nani?
Mkurugenzi wa VETA : Ndio najua.
Kaimu Mwenyekiti   : Inawajibika wapi?
Mkurugenzi wa VETA : Kwa waziri.
Wajumbe wa kamati  : Ahaaa!
Kaimu Mwenyekiti   : Unajua kweli?
Mkurugenzi wa VETA : Ndio
Kaimu Mwenyekiti   : Wapi tuambie?
Mkurugenzi wa VETA : Kwa Kamati yako Mwenyekiti (yaani POAC).
Wajumbe wa Kamati  : Ahaaaa!

Kutokana na mahojiano hayo wajumbe wa Kamati hiyo, walibaini kwamba  Mkurugenzi Mkuu wa VETA hajui bodi yake inawajibika kwa nani jambo ambalo ilibidi asaidiwe na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw.Idrisa Mshoro, aliyeingilia kati mahojiano hayo kwa kusema

Mwenyekiti wa Bodi : Bodi inawajibika kwa CAG Mheshimiwa Mwenyekiti

Kamati hiyo pia ilisikitishwa na tabia ya mamlaka hiyo kubadilisha mtaala kwa wanafunzi huku sh. bilioni 13 zikitumika kama matumizi mengine (OC) bila kuorodheshwa kwenye kitabu kama inavyotakiwa.

Akijibu ongezeko la matumizi hayo Mkurugenzi wa fedha wa mamlaka hiyo Bi.Neema Mwakalukwa, alisema wanaratibu vyuo zaidi ya 900 nchi nzima na kwamba idadi ya wanafunzi ilipanda kutoka 26,000 mwaka 2008 hadi kufikia 60,000 mwaka 2010.

Hata hivyo mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alisema tabia ya kubadilisha mitaala kila mara ni sawa na watu wanaochezea sanamu maarufu kama Joyce wowowo, hivyo kuwafanya wabunge kuguna.

No comments:

Post a Comment