Na Peter Mwenda,Igunga
WATU nane wanaosadikiwa kuwa walinzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamempiga mwandishi wa habari wa gazeti la Dira Mtanzania kwa kile kinachodaiwa aliandika habari za kukiponda chama hicho na kumdhalilisha Katibu wa Fedha na Uchumi Bw. Mwigullu Nchemba.
Akisimulia mkasa huo mwandishi huyo, Bw. Mussa Mkama alisema tukio la kupigwa lilimpata Jumamosi saa 1 usiku akiwa na mwandishi mwingine Bw. George Maziku baada ya kumaliza mahojiano na Mbunge wa Viti Maalum Vijana Jimbo la Bunda, Bi. Easter Bulaya katika hoteli ya The Peak ambako wanafikia viongozi wa CCM.
"Baada ya kumaliza mahojiano yetu na Bulaya wakati tukitoka getini niliwaaga walinzi nikiwambia sasa nimemaliza kazi yangu naondoka, mara niliitwa na mtyu mmoja aliyevalia sare za CCM mara baada ya kumkaribia nilizingirwa na kupigwa mateke na ngumi hadi kudondoka hawakuishia hapo waliendelea kunipiga"alisema Bw. Mussa.
Alisema mwandishi wenzake aliyekuwa naye Bw. Maziku akiasaidiwa na mtu mwingine walifanikiwa kuwatuliza walinzi hao ndipo alipopata nafasi ya kukimbia na kwenda kituo cha polisi cha Igunga kutoa taarifa.
Bw. Mussa alisema baada ya kutoa taarifa alikwenda hospitali ili kupata matibabu lakini ameumia mkononi, shavuni na sehemu za mbavu ambako walimpiga mateke hata baada ya kudondoka.
Alisema mahojiano na Bi. Easter yalihusu tukio la mbunge huyo kudai kutupiwa risasi na Mratibu wa kampeni za Chadema Bw. Mwita Mwikabe kwa kile alifchodai CCM kuharibu mikakati ya chama hicho ya kukusanya shahada za kupigia kura.
"Nadhani sababu kubwa ya mimi kupigwa ni zile habari zangu katika gazeti la Dira Mtanzania la Jumatatu iliyopita likiwa na bahari mbili kubwa, ya kwanza ni ile ya CCM aibu tupu Igunga ikieleza kufumaniwa kwa Mratibu wa Kampeni za CCM, Bw. Nchemba na nyingine ikisema kuwa CCM yakiri Rostam Kiboko" alisema Bw. Mussa.
Alisema katika tukio hilo amepoteza vifaa vya kutendea kazi yake na fedha taslimu sh. 450,000 ambazo zilikuwa katika pochi yake
Mratibu wa Kampeni Bw. Nchemba alipoulizwa kuhusu walinzi wake kumpiga mwandishi alisema hana taarifa hizo,Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Igunga, Bw. alisema hajapokea taarifa za mwandishi huyo.
Katika tukio jingine Mwenyekiti wa wazee wa CUF, Bw.Salum Masanja ameruhusiwa kutoka hospitali ya Wilaya ya Igunga baada ya kupigwa na mabaunsa wa CCM waliokuwa katika msafara wa Katibu Mkuun wa UVCCM, Bw. Martin Shegela Jumanne iliyopita.
Msemaji wa CUF, Bw. Silas Bwire alisema Mwenyekiti huyo wa CUF aliyepigwa na wafuasi wa CCM wakati akipandisha bendera ya CUF katika kijiji cha Iyogelo chama chake kitasimamia kesi hiyo mpaka ukwelin ubainike wahusika waliompiga.
CUF ambacho kiko katika kampeni zake za chini kwa chini, nyumba kwa nyumba, mikutano ya hadhara kimewataka wananchi wakichague chama hicho kwa sababu ndicho pekee chenye kuhubiri amani kwa watanzania wote bila kujali itikadi.
Meneja wa Kampeni wa CUF. Bw. Antony Kayange alisema vyama vinavyowapiga viongozi wa vyama vingine,wanachama wao na kumwagia watu tindikali wataendeleza visasi baada ya mbunge wa chama chao kuchaguliwa.
Mgombea Ubunge wa CUF, Bw. Leopold Mahona alisema imefika wakati CCM iache madaraka kwa upinzani ili walete maendeleo kwa wananchi wa Igunga ambao maisha yao ni duni na ya kubahatisha.
Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Bw. Julius Mtatiro akihutubia wananchi wa Igunga katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Sokoni mjini hapa alisema chama chake kitachukua jimbo la Igunga kwa sababu kwanza inao mtaji wa kura 11,321 alipopata mgombea wao mwaka 2010 na kinakubalika kwa vwananchi kwa sababu hakina vurugub wala siasa za chuki.
Alisema katika kampeni zao katika Kata 26 za Igunga wananchi wameahidi kuwapigia kura za ndiyo kwa sababu ya kuhutubia amani na utulivu kwa watanzania kunakofanywa na chana hicho katika kampeni zake.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Bw.Phillip Mangula amewataka wananchi wa Igunga wakipigie kura chama hicho kwabsababu kimeleta maendeleo makubwa kutoka upatikane uhuru nchini.
Bw. Mangula akihutubia mkutano wa kampeni katika kata ya Mwamasunga katika kata ya Igunga alisema wakati wa uhuru hakuna mtanzania aliyemiliki baiskeli ikilinganishwa na sasa hivi ambako kila mmoja anao uwezo wa kununua.
Alisema wakati huo pia mkoa wa Tabora kulikuwa na shule mmoja ya Sekondari lakini sasa hivi kuna shule zaidi ya 154 katika mkoa wa Tabora.
Hata hivyo wananchi hao walitoa masharti kwa CCM wamlete mgombea ubunge wa Jimbo la Igunga, Dkt. Dalaly Kafumu akawaahidi wananchi hao jinsi atakavyotatua matatizo yanayowakabili ya uhaba wa maji, masoko ya mazao yao na upatikanaji wa pembejeo.
“Puuzeni uchochezi unaofanywa na wamnasiasa ili kuenzi amani na utulivu vilivyopo nchini’”alisema Bw. Mangula.
Wananchi hao walisema hawako tayari kupewa ahadi hewa kama alizowahi kutoa mbunge aliyejiuzulu, Bw. Rostam Aziz aliyejivua gama kutoka CCM.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment