TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION
TANGAZO SHIWATA
Wednesday, 31 August 2011
Algeria kutua Alhamisi usiku,Rwiza,Chaula wateuliwa Kamati ya kutathimini waamuzi
Timu ya Taifa ya Algeria (Desert Warriors) itawasili Septemba Mosi mwaka huu saa 2.50 usiku kwa ndege maalum. Algeria itacheza mechi ya mchujo kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Equatorial Guinea na Gabon.
Mechi hiyo itachezwa Septemba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Viingilio kwa mechi hiyo ni viti vya kijani ni sh. 3,000, viti vya bluu sh. 5,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 7,000, VIP C sh.10,000, VIP B sh. 20,000 na VIP A sh. 30,000. Tiketi zitaanza kuuzwa Septemba Mosi mwaka huu.
Vituo vya kuuza tiketi ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha Mafuta cha Big Bon (Kariakoo), Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Samora na Ohio, Uwanja wa Uhuru na Kituo cha Mafuta cha OilCom Ubungo.
Mchezaji Idrisa Rajab anayechezea Sofapaka ya Kenya amewasili jana usiku na tayari ameripoti kwenye kambi ya Taifa Stars. Stars inaendelea na mazoezi Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.
MASHITAKA DHIDI YA RAGE, SENDEU
Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti wake Alfred Tibaigana iliyokuwa ikutane jana kusikiliza malalamiko dhidi ya Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage na Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu imeahirisha kikao chake.
Kwa mujibu wa Tibaigana, kikao kimeahirishwa kutokana na Kamati kutotimiza akidi (column) kwa wajumbe wake. Walalamikiwa wataarifiwa siku ambayo kikao kitapangwa tena.
IVAN KNEZEVIC AOMBEWA ITC
Aliyekuwa kipa wa Yanga, Ivan Knezevic ameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) na Chama cha Mpira wa Miguu cha Serbia (FAS) ili kujiunga na klabu yake mpya nchini humo.
Knezevic ameombewa ITC kama mchezaji wa ridhaa katika klabu ya FK Borac ya nchini humo. TFF itampatia hati hiyo kwa vile mkataba wake katika klabu ya Yanga ulikuwa umemalizika.
11 WATEULIWA KUTATHMINI WAAMUZI
Kamati ya Waamuzi ya TFF imeteua watathmini 11 wa waamuzi (referees assessors) kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom. Watathmini hao watasimamia baadhi ya mechi za ligi hiyo.
Walioteuliwa ni Alfred Lwiza (Mwanza), Soud Abdi (Arusha), Charles Mchau (Kilimanjaro), Manyama Bwire (Dar es Salaam), Joseph Mapunda (Ruvuma), Isabela Kapela (Dar es Salaam), Paschal Chiganga (Mara), Emmanuel Chaula (Rukwa), Mchungaji Army Sentimea (Dar es Salaam), David Nyandwi (Rukwa) na Leslie Liunda (Dar es Salaam).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment