TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Tuesday, 19 July 2011

Mvungi, Mbatia na Mziray wapongeza wabunge mjengoni

Na Peter Mwenda
MSIMAMO wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kupinga kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini umepongezwa kumtaka Waziri Bw. William Ngeleja na Katibu wake Mkuu, Bw.David Jairo.

Dkt. Sengondo Mvungi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema jana kuwa bunge limeelewa kazi yake kwani limeanza kujua thamani na heshima wanayostaili watanzania kuwa nayo.

Alisema kwa mara ya kwanza wabunge wamezungumza kwa majonzi na uchungu mkubwa wa hali waliyonayo watanzania na kuongeza kuwa bunge kama hili lingekuwepo Tanzania ingepiga hatua kubwa ya maendeleo.

"Tangu awamu ya tatu tulizungumzia paka asiyekamata panya ambayo ni Kampuni ya Net Group Solution haikuja na kipuri wala senti moja lakini walichota fedha zetu wakaondoka, tatizo la umeme lilianza kuonekana kuwa kubwa kutoka serikali ya awamu ya tatu"alisema Dkt. Mvungi.

Alisema ili kufikia malengo ya milenia Tanzania inatakiwa kuzalisha megawati 6,000 mpaka megawati 7,000 kutokana na utajiri wa gesi iliyopo nchini.

"Mitambo iliyonunuliwa kwa ajili ya kufunga Dar es Salaam kwanini isiende kufungwa Songosongo inapotoka gesi,hiyo ni akili ya kizembe kwa tatizo kubwa la umeme kama hili"alisema Dkt. Mvungi.


Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Bw. James Mbatia alisema hatua imefikiwa na bunge imetokana na uzembe wa viongozi wa Serikali ya CCM.

Alisema tatizo la mahitaji makubwa ya umeme ni la muda mrefu kutoka miaka ya 1980 wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere lakini halikufanyiwa kazi kitaalamu.

Alisema bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ni chafu iliyojaa makosa mengi ambayo haistahili kupitishwa kwa maslahi ya watanzania.

Bw. Mbatia alisema msimamo wa wabunge kuigomea bajeti hiyo umeonesha dhahiri kuwa mchele ni upi na pumba ni zipi kwa sababu haiwezikani Tanzania ishindwe kuwa na umeme wa kutosha wakati imejaliwa kuwa na gesi,makaa ya mawe na Uranium.

Alisema kama Serikali ingekuwa makini hata kuvuna maji ya kutosha kipindi cha masika kwa ajili ya kuzalisha umeme ungefanikiwa kuzalisha umeme wa kutosha.

Alisema Tanzania inayo gesi ya kuzalisha umeme wa kutosha na kuuza nchi nyingine za jirani,kuzalisha umeme kutumia makaa ya mawe lakini tatizo kuwa wataalamu hawapewi nafasi ya kuonesha uwezo wao.

Mwenyekiti wa APPT Maendeleo Bw. Peter Mziray alisema kabla ya bunge hili wabunge waliokuwepo walikuwa wakipitisha hoja hata kama inawaumiza watanzania.

Alisema kitendo cha Katibu Mkuu Bw, Jairo kutaka taasisi za wizaya hiyo kuchangia sh. mil. 50 kwa ajili ya kutoa hongo kwa wabunge ni kosa ambalo TAKUKURU inatakiwa imkamate na kumfungulia mashtaka haraka.

Alisema hiyo ni aibu kwa watanzania kwa sababu baraza la mawaziri na watendaji wao ni jipya na waliaminika lakini kutokana na kasoro hizo ni feki hivyo livunjwe.

Bw. Mziray alisema Waziri Ngeleja na Katibu wake Mkuu Bw. Jairo wajing'atue madarakani haraka kabla ya Rais Kikwete kurejea nchini.

Alisema wakati Serikali inatafakari kutafuta njia mbadala ya mgawo wa umeme waingize vifaa vya umeme wa jua yaani sola bila kutoza ushuru ili angalau baadhi ya huduma ambazo hazihitaji umeme mwingi ziendelee.

Alisema kutokana na hali tete ya upatikanaji wa umeme vifaa vya sola vinaweza kusaidia kutumika kama vibatari ili kupata mwanga wa kufanya shughuli nyingine ndogondogo ziendelee.

Alisema kutokana na hali hiyo kufikia hali ngumu ya kuendelesha maisha ya kila siku ya wananchi siku ambayo watanzania wakiamua kufanya maandamano ya mgawo wa umeme ndiyo siku ambayo Rais Kikwete ataachia madaraka.

mwisho.



 

No comments:

Post a Comment