TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Monday, 18 July 2011

Askofu Nzigilwa avipasha vyombo vya habari

Na Peter Mwenda

ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa ametoa wito kwa vyombo vya habari nchini kuandika matukio mema yatakayobadilisha sura ya watanzania.

Akizungumza katika ibada ya Kipaimara iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kitunda juzi, Mhashamu Nzigilwa alisema kwa vile vyombo vya habari vinaandika habari nyingi za maovu mbalimbali yanayotokea nchini zinaitangaza Tanzania vibaya katika sura ya kimataifa.

Alisema nchi za Magharibi zilikuwa zikiandika habari za Afrika zile ambazo si nzuri na kuficha zile ambazo ni njema.

Alisema kutokana na kasumba hiyo vyombo vya Tanzania navyo vimeiga kawaida hiyo na sasa habari zote njema na zenye kutoa mafunzo katika jamii hazipewi uzito.

Mhashamu Nzigilwa alisema ili jamii ijenge maisha imara ni lazima wazazi wajenge mfumo wa kuacha kuonesha vitendo viovu kwa watoto wao ambao nao huiga kutoka kwa wazazi.

Alisema watoto 145 waliopata kipaimara katika kanisa hilo wawe mfano katika familia zao kwa kuchukia ujumbe wenye kupotosha kama vile kuruhusu picha za ngono na ambazo hazina ujumbe mwema.

Akitoa salamu za kanisa hilo, Paroko wa Kitunda, James Mweyunge alisema ujumbe wa Askofu ufanyiwe kazi na kuahidi kutoa mafunzo kwa waumini kufuata yale anayoyataka Mungu ya kuacha matendo mabaya.

Awali katika risala ya vijana waliopata kipaimara, waliomba Serikali kuchukua hatua kali kwa wale wote wanaoiba mali umma, wanaotupa watoto na isaidie kuondoa matatizo ya watoto wa mitaani.

mwisho.

No comments:

Post a Comment