Na Peter Mwenda
WALEMAVU wa Ngozi wameathirika na losheni wanazopaka kuwakinga na mionzi ya jua kwa kuwatoa vidonda na kuwasababishia uono hafifu.
Mwenyekiti wa Chama cha Albino wilaya ya Kinondoni, Bw. Musa Geuza alisema jana losheni ambazo zinaingizwa kutoka nje ya nchi nyingine zimewatoa vidonda na wengine kudhurika kwa kuwasababisha macho kutoona kulikosababishwa na kutokuwa na daktari wa maalum wa kuchunguza afya zao.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Utendaji wa Chama cha Albino wilaya ya Kinondoni (C.C.A.T) alisema losheni za Nevea Body,Coppertone kutoka Canada zinasaidia sana albino lakini nyingine zimekuwa zikiwaathiri.
Alisema bei ya losheni hizo ni ghali ambazo albino hawezi kumudu kununua kwani bei yake inaanzisha sh. 30,000 hadi sh. 60,000 kwa losheni yenye ujazo wa mil.220.
Naye Mwenyekiti wa albino wilaya ya Temeke Bw. Kassim Kibwe alisema amewahi kutumia losheni ambayo (jina tunalo) ambayo ilimfanya ashindwe kuona na mpaka sasa haoni vizuri baada ya kupaka usoni.
"Losheni za albino tunapaka ili kuzuia mionzi ya jua usituathiri ngozi yetu, lakini nyingine zinatufanya tubadilike rangi kuwa njano na wengine wanapata vidonda sehemu ambazo zinachomwa jua" alisema Bw. Leonard Kidole ambaye ni Katibu wa CCAT wilaya ya Kinondoni.
Bw. Kidole alisema imefika wakati Serikali igharamie matibabu kwa albino na kutoa miwani bure ili kuwajengea uwezo wa kusoma na kuishi kama binadamu wengine.
Alisema albino pia wanahitaji kusaidiwa kupewa kofia za kuzuia jua,miamvuli na kupewa daktari ambaye atakuwa anachunguza afya za albino badala ya kuachia Taasisi ya Saratani Tanzania ya Ocean Road ambako imelewa na wingi wa wagonjwa wa saratani.
Wakati huo huo albino wa wilaya ya Kinondoni wamepata mafunzo ya utawala na uandishi wa vitabu na uanzishaji wa vitabu vya kumbukumbu ya hesabu za fedha.
Bw. Geuza alisema mafunzo hayo ya wiki moja yaliyofanyika Bagamoyo mkoa wa Pwani na kufadhiliwa na The Foundation for Civil Society, albino hao walisema mafunzo hayo yamewasaidia kujua mipaka wa uongozi na kutunza kumbukumbu za mapato na matumizi ya fedha.
mwisho.
No comments:
Post a Comment