Na Peter Mwenda
WIZARA ya Kilimo Chakula na Ushirika imefikia makubaliano na Shirika la Rice Afrika ya kuzalisha mbegu na kufanya utafiti wa zao la mpunga liwe la chakula na biashara.
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa katika makubaliano hayo Shirika la Rice Afrika kushirikiana na wizara yake wamekubaliana kuongeza uzalishaji wa mpunga kutoka tani 900,000 kwa mwaka kufikia tani mil 2.7 mwaka.
"Tumekubaliana kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa mpunga kutosheleza chakula nchini na kuuza nje ya nchi kutoka tani zinazozalishwa ziongezeke mara tatu mpaka nne " alisema Profesa Maghembe.
Alisema wizara yake itachagua baadhi ya mbegu za kulima kutoka mbegu aina 30,000 za mbegu ambazo zinafaa kulimwa nchini na tayari mashamba yametengwa kwa ajili ya kilimo cha mpunga.
"Pia tumeweka msukumo katika kilimo cha umwagiliaji na kilimo cha mpunga wa mlimani, tutachukua kila hatua ya kuanzia kilimo mpaka kuvuna" alisema Profesa Maghembe.
Alisema wataalamu wa Rice Afrika wanawasili nchini Januari kuungana na maofisa wa wizara hiyo kuanza kazi rasmi ya kufanya utafiti na kuzalisha mbegu.
Alisema kinachokusudiwa ni ekari moja izalishe tani 5-7 badala ya sasa ambako ekari moja inazalisha tani moja ya mpunga.
No comments:
Post a Comment