MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kisarawe kupitia CCM,Bw. Seleman Jafo amewataka wanachama wenzake wa chama hicho kuvunja makundi.
Bw. Jaso alitoa kauli hiyo wakati akitoa salamu za shukurani baada ya kuchukua fomu za kugombea ubunge wa jimbo hilo na kusindikizwa kwa maandamano na wanachama waliongozwa na Kaimu Katibu wa CCM wa wilaya ya Kisarawe Bw. Mustafa Dikoroma.
"Nawaomba wenzangu waliowashindwa kwenye kampeni ya kura za maoni kuniunga mkono mimi na chama chetu ili kiweze kuibuka na ushindi wa kishindo kuanzia madiwani, wabunge na Rais Kikwete" alisema Bw. Jafo.
Alisema kuteuliwa kwake kunafungua ukurasa mpya wa kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo ambao wana kiu kubwa ya kupata maendeleo kulingana na wilaya nyingine katika sekta za elimu,afya,miundombinu na kilimo cha kisasa.
Katika shamrashamra hizo Katibu wa umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani hapa Bi.Mwajuma Mombwe alisema amekubali kuvunja kambi yake kwa sababu hakuwa anamuunga mkono mgombea huyo hivyo atashirikiana naye kupigia kampeni CCM.
Jumuiya nyingine zilizomsindikiza Bw. Jafo ni pamoja ni Wazazi na Umoja wa Vijana (UVCCM)wilaya ya Kisarawe.
Awali Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kisarawe Bw. Isaya Moses alisema hadi kufikia jana ni vyama vitatu ndivyo vichukua fomu za kugombea ubunge.
Alisema vyama ambavyo vimechukua fomu hizo ni Tanzania Labour Party (TLP),CHADEMA na CCM.
No comments:
Post a Comment