TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Thursday 26 November 2015

SHIWATA kugawa nyumba 14 Mkuranga, yampongeza Dkt. Magufuli kumteua Majaliwa Waziri Mkuu

Na Peter Mwenda

MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA)umeandaa mkutano wa wanachama wake Jumamosi kutangaza majina ya wanachama watakaokabidhiwa nyumba 13 na misingi ya nyumba 14 katika kijiji cha Mwanzega, Mkuranga.

Mwenyekiti wa SHIWATA,Cassim Taalib alisema jana Dar es Salaam jana kuwa mkutano huoutakaofanyika Ilala, Bungoni Dar es Salaam kuanzia saa 4 pia watatangazwa viongozi watakaoshika nafasi za uongozi zilizo wazi.

Nafasi za uongozi zilizo wazi ni Makamu Mwenyekiti iliyokuwa ikishikiliwa na Marehemu Kepteni John Komba,Katibu ambayo ilikuwa inashikiliwana Selemani Pembe ambaye yupo India kikazi na Mweka Hazina ambaye Flowin Nyoni ambaye ni Mhadhiri wa Chuko Kikuu cha Dodoma.

Katika hatua nyingine SHIWATA imeupongeza uongozi wa Rais John Pombe Magufuli kumteua Mkufunzi wa Mpira wa Miguu wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Majaliwa Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.

Alisema medani ya michezo inahitaji msukumo wa viongozi wanaojua michezo hivyo ni kipindi cha kujiandaa kuiletea sifa Tanzania kupitia michezo ya soka, ndondi, riadha,netiboli na mingine katika michezo ya Afrika Mashariki,Michezo ya Afrika, michezo ya madola na michezo ya dunia.

Taalib alisema ili kuonesha viongozi wetu wapya ni wapenda michezo hivi karibuni Rais Magufuli alikubali kuwa mgeni rasmi katika pambano la kuwania kucheza kombe la dunia kati ya Stars na Algeria kwenye uwanja wa Taifa ambapo alimtuma Makamu wa Rais, Suluhu Samia Hassan kumwakilisha hiyo inaonesha Tanzania imepata viongozi wapenda michezo.

Alisema wasanii na wanamichezo watapiga hatua kubwa mbele kwenye uongozi wa Dkt. Magufuli kwani kuna kila dalili kuwa kazi zao zitathaminiwa na kupewa kipaumbele.

Taalib alisema mtandao wa SHIWATA ambao unajumuisha wanamichezo, wasanii, waigizaji, waandishi wa habari na wasanii wa kazi za mikono wamemkubali Dkt. Magufuli kwa kasi aliyoanza nayo ya kufuatilia mambo hasa kuondoa kero za wanyonge ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa hawapati huduma muhimu za kijamii za elimu na afya.

Alisema wasanii wanaimani kubwa na Dkt. Magufuli kwani ni mchapakazi na mtu asiyependa wananchi wake wadhulumike wakiwemo wasanii ambao walizunguka nchi nzima kwenye kampeni zake na kujionea shida za wananchi zinazowakabili wakiomba mahitaji mbalimbali katika nchi yao yenye rasilimali lukuki.

SHIWATA yenye wanachama zaidi ya 8,000 nchini inamiliki hekari 300 za kujenga nyumba za makazi wa bei nafuu ambako nyumba 120 zimekwisha jengwa katika kijiji cha Mwanzega Mkuranga na hekari 500 zilizotengwa kwa ajili ya kilimo zimelimwa na kupanda mazao mbalimbali katika kijiji cha Ngarambe Mkuranga.
 

mwisho





No comments:

Post a Comment