TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Thursday 3 September 2015

Kasi ya ujenzi uwanja wa ndege JNIA yaikuna Serikali

Na Peter Mwenda

SERIKALI imepongeza kasi ya ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ambao umefikia asilimia 90.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Shaaban Mwinjaka akipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa kasi nzuri ya ujenzi huo jana Dar es Salaam alisema kazi hiyo ni nzuri tofauti na zilivyo taasisi nyingine.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri,ripoti inaoana na kazi halisi inayoendelea huko,siyo kama wengine wanakupa ripoti josho limejengwa ukienda hulikuti” alisema Dkt. Mwinjaka.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa fupi ya maendeleo ya ujenzi huo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mradi huo, Mhandishi Mohammed Millanga alisema kazi ya ujenzi wa mradi huo unaogharimu sh. Bilioni 518 inaendelea kwa kasi kubwa na awamu ya kwanza ikitarajiwa kukamilika Juni 2016.

Mhandisi Millanga alisema jengo hilo limekamilika kwa 96, uwekaji vyuma 90%, matofali ya kuta 80%, uezekaji paa 60%, uwekaji vioo 25%, mifumo ya maji 80%,  umeme na mabomba 30% na maegesho ya magari 75% na ya ndege 30%.

Mhandisi Millanga alisema mradi huo pia unakabiliwa na changamoto mbili kubwa ya huduma ya visima vya mafuta ya ndege na ukosefu wa fedha za kumalizia mradi na wameomba fedha serikalini na wanatafuta mwekezaji wa kisima cha mafuta.

Katibu Mkuu, Dkt. Mwinjaka ameahidi Serikali kutoa fedha za kumalizia mradi huo.Awamu ya pili itakayochukua abiria milioni 2.5 itakamilika 2017. Ya kwanza ya abiria 3.5 itaisha Juni 2016.

Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Suleiman Said Suleiman alisema mradi huo utakuwa na hadhi kama ya viwanja vingine vikubwa duniani cha Heathrow cha Uingereza, Dubai cha Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwani ndege zinazohudumiwa huko kama Emirates ndizo zitakuja hapa kwani patakuwa na miundombinu ya aina hiyo hiyo.

Katika hatua nyingine baada ya kumalizika kwa jengo hilo, treni maalum itaanzishwa na Serikali kusafirisha abiria wawahi kwenda na kutoka katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) wanaposafiri na pia kwenda maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Mwinjaka alisema Serikali inatarajiwa kutumia bilioni 2.9 kufanya upembuzi yakinifu kupata gharama za kuanzisha treni hiyo.

Alisema treni hiyo ndogo (siyo kama ya Mwakyembe) itaendeshwa na sekta binafsi ikitumia injini za Ashok Leyland.

Alisema njia itakazotumia ni Dar kwenda Mwakanga hadi Pugu  kupitia Kiwanja cha Ndege, Dar kwenda Ubungo hadi Kibaha, Dar kwenda Mwenge hadi Bunju, Dar kwenda  Mivinjeni hadi Mkuranga na  Dar kwenda  NSSF Bridge hadi Kigamboni.

mwisho


No comments:

Post a Comment