TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Monday 20 July 2015

Banza Stone afariki dunia

Na Mwandishi Wetu

MWANAMUZIKI mkongwe nchini Ramadhani Masanja ‘Banzastone’ amefariki dunia nyumbani kwao Sinza njia panda Lion jana mchana.
Banzastone amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu  huku akipelekwa hospitali na kutibiwa nyumbani kwa tiba za aina mbalimbali.
Taarifa rasmi za kifo cha mwanamuziki huyo zilitolewa jana na kaka yake Khamis Masanja .
Masanja alisema kwamba  kifo cha Banzastone kimekuja baada ya kuugua kwa muda mrefu ambapo alikuwa akisumbuliwa na kifua pamoja na fangas za kichwani.
Aidha kaka huyo wa marehemu alisema kwamba taratibu za mazishi zinafanyika kwa kuzingatia familia yao ilivyokua kubwa  hivyo taarifa zaidi zitatolewa hapo baadaye.

Naye  Mkurugeni wa Kampuni ya The African Stars Entertainment (ASET),Asha Baraka alisema kwamba amepokea kwa majonzi makubwa taarifa za msiba huo kwani yeye amekuwa katika mstari wa mbele katika kupigania uhai wa mwanamuziki huyo aliyekuwa mahiri katika utunzi na kuimba pia.

Itakumbukwa kwamba Banzastone ni kati ya wanamuziki waasisi wa bendi ya Twanga Pepeta ambapo pia atakumbukwa kwa kuachia vibao kadhaa ikiwemo Kumekucha, Angurumapo Simba, Mtu Pesa, na wimbo wake mmoja ambao aliuachia wakati akiwa na bendi ya Twanga  Chipopolo aliachia wimbo wa ‘Hujafa Hujasifiwa’ ambao katika mashairi yake alijiimba yeye mwenyewe huku akisema siku akifa atasifiwa sana wengine watamwita teja na mambo mengi alizungumza katika wimbo huu.

Mapema mwezi huu Banzastone alilazwa katika Hospitali ya Mwananyamala , Kinondoni Jijini Dar es Salaam kabla ya kupata ruhusa ya kurudi nyumbani. shughuli za msiba zitakuwa nyumbani kwao Sinza  njia panda Lion Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment