TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Wednesday 4 March 2015

Komba alikuwa Makamu Mwenyekiti SHIWATA

Na Peter Mwenda

MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) unaungana na watanzania wote kuomboleza kifo cha Makamu Mwenyekiti wao, John Komba aliyefariki Jumamosi na kuzikwa jana nyumbani kwao kijiji cha Litui, Mbinga mkoa wa Ruvuma.

Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib katika salamu zake za rambirambi alisema mtandao huo umempoteza kiongozi mwadilifu aliyetumia kipaji chake cha usanii kuwaunganisha makundi ya wanamichezo,waigizaji, wasanii wa luninga, bongo movie,wacheza sarakasi na waandishi wa habari kuunda mtandao huo.

Alisema Kepteni Komba siku zote za maisha yake aliamini sanaa ni mkombozi wa wanyonge katika jamii ambako alitumia fani yake ya ualimu kufundisha wasanii wa fani mbalimbali alipokuwa na kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT), aliunda Kwaya, maigizo, sarakasi, taarab na muziki wa dansi.

Marehemu Komba akiwa na kikundi chake cha TOT aliibua vipaji vya wasanii mbalimbali waliotamba zamani na wengine bado wanaendelea kutamba katika kama Nasma Hanisi Kidogo, Laila Khatib, Sheba Juma, Selemani Pembe, Banza Stone, Mohamed Mrisho, Badi Makule, Ali Star, Khadija Kopa, Othman Sudi, Abdul Misambano, Mwanamtama Hamisi na Haji Boha.

Taalib alisema SHIWATA imempoteza kiongozi aliyekuwa msaada mkubwa katika kuimarisha mtandao huo kwa hali na mali na kuwashawishi wasanii wake wa TOT kujiunga na mtandao huo ili kushirikiana katika kujenga kijiji cha wasanii cha Mwanzega, Mkuranga.

Marehemu Komba ambaye alikuwa mwanachama mwenye kadi namba moja wa SHIWATA kati ya wanachama 8,000 wa mtandao huo alikuwa akilipia michango yake na kuwa mfano kwa wengine.

Taalib alisema SHIWATA imewapoteza wanachama maarufu katika kipindi cha karibuni na hivyo kuongeza pengo katika utendaji wake kama Ibrahim Muchacho, Fundi Said (Mzee Kipara), Seteven KAnumba, Hamisi Amigolas na Amina Ngaluma.

Alisema katika uongozi wa marehemu Komba amesaidia kujengwa kwa nyumba 104 za wasanii katika kijiji cha Mwanzega ambapo wasanii wanaendelea na ujenzi.

mwisho

No comments:

Post a Comment