TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Wednesday 12 November 2014

SHIWATA YALIA KUMPOTEZA AMIGOLAS

Na Peter Mwenda

MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA)unaungana na watanzania kuomboleza kifo cha mwanamuziki maarufu Hamisi Kayumbu 'Amigolas' aliyefariki Jumapili na kuzikwa Jumatatu iliyopita katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib alisema jana Dar es Salaam kuwa marehemu Amigolas atakumbukwa kwa mengi aliyoyafanya akiwa mwanachama wa mtandao huo alishiriki kutafuta eneo la makazi ya wasanii ya kijiji cha Mwanzega na shamba la wasanii lililopo Ngarambe wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani.

Alisema alikuwa kiongozi wa mstari wa mbele pale  alipowahamamisha wanamuziki wenzake kujiunga SHIWATA kutoka bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta'akiwemo Luiza Mbutu,marehemu Abuu Semhando na wengine.

Marehemu Amigolas alifariki kwa ugonjwa wa moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (M.N.H) alipokuwa amelazwa kwa siku tano kabla mauti kumkuta Jumamosi saa tano usiku.

Mkurugenzi wa African Stars 'Twanga Pepeta', Asha Baraka aliyekuwa mwajiri wake kabla ya kuhamia bendi ya JKT Ruvu alisema marehemu alikuwa mwanamuzi aliyejituma na kufanya kazi kwa juhudi zote kutoka ajiunge na bendi hiyo mwaka 1997.

Hivi karibuni SHIWATA imepoteza wanachama wake maarufu waliofariki akiwemo Abuu Semhando,Amina Ngaluma na Muhidin Gurumo.

Marehemu Amigolas alizikwa na umati mkubwa wa waombolezaji kwenye makaburi ya Kisutu Jumatatu saa 10 jioni. Ameacha wajane wawili na watoto wanne. Mungu ilaze roho marehemu mahali pema peponi. Amen.

No comments:

Post a Comment