Waandishi
wa habari wakimchukua picha kwa mama mkubwa Nasra, Mariamu Saidi (38)
mara baada ya kufikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Morogoro wakati
wa kusikiliza kesi inayomkabili ya kula njama na kumtesa Nasra Rashidi
(4) wakati wa uhai.
Umati wa watu, wengi wao wakiwa wanawake jana ulifurika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, kufuatilia kesi ya kula njama na kumfanyia vitendo vya ukatili mtoto Nasra Rashid (4) wakati wa uhai wake inayowakabili watu watatu. Washtakiwa waliofikishwa mahakamani ni mama mkubwa wa marehemu, Mariamu Said (38) na mumewe, Omary Mtonga (30) na baba mzazi wa Nasra.
Rashid Mvungi (40). Mara baada ya kufika mahakamani hapo, watu waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo waliwapokea kwa kuwazomea huku baadhi ya kina mama wakiangua vilio.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na kosa la kumtendea ukatili Nasra ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni Mosi, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam kwa kumweka ndani ya boksi kwa miaka mitatu.
Umati wa watu ulianza kufurika katika viunga vya mahakama mapema asubuhi huku kukiwa hakuna ulinzi wakati huo na kuingia ndani ya mahakama hiyo ya wazi na kuketi kwenye madawati wakisubiri.
Washtakiwa walifikishwa hapo saa 4:20 asubuhi kwa gari la polisi aina ya Land Lover Defender na kupokewa na watu hao kwa zomeazomea na vilio.
Kwa kuwa Mahakama hiyo haina mahabusu ndogo kwa ajili ya washtakiwa wa kike, baada ya kuteremshwa kwenye gari, Mariamu aliwekwa chini ya mti na kundi la watu lilimzingira na kuanza kumzomea huku baadhi ya wanawake wakiangua vilio na kumtolea maneno makali jambo lililowafanya polisi wamwondoe na kumwingiza kwenye moja ya vyumba vya mahakama.
Muda wote kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea, shughuli nyingine za mahakama zilisimama kwa muda kutokana na kelele za watu hao.
Pamoja na jitihada za askari polisi za kuwazuia watu hao kusogea kwenye mahakama hazikufanikiwa kwa kiwango kikubwa kwani wengine waliingia ndani na baadhi kubaki nje wakisikiliza kwa makini kesi hiyo iliyokuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo.
Baada ya polisi kutuliza hali katika viwanja hivyo, Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Sunday Hyera akisaidiwa na Mwanasheria mwenzake, Edgar Bantulaki na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Joseph Zablon, alidai kuwa kesi hiyo ilikuwa katika hatua ya kusikilizwa kwa maelezo ya awali ya shtaka la kula njama na kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto.
Alisema upande wa mashtaka umepata taarifa kuwa muathirika wa tukio hilo, Nasra Mvungi alifariki dunia Juni Mosi, mwaka huu... “Hivyo kwa kuzingatia mabadiliko hayo, upande wa mashtaka unaiomba Mahakama kutoa ruhusa kwa washtakiwa wote watatu kwenda polisi ili wakahojiwe na kutoa maelezo yao upya ili hatimaye, kuuwezesha upande huo kuandaa hati nyingine ya mashtaka kwa mujibu wa sheria.”
Pia aliiomba Mahakama kusitisha usikilizaji wa awali wa kesi hiyo na kupanga tarehe nyingine ya kuitaja.MWANANCHI
No comments:
Post a Comment