Na Peter Mwenda
WANANCHI wa vijiji 10 vya Kata ya Magara wilayani Manyara wamemwandikia barua Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kulalamikia kuporwa ardhi yao.
Wakizungumza Dar es Salaam jana wananchi hao Bw. Tarmo Tambo na Bw. Mussa Sule waliowakilisha wenzao 2,500 walidai kuwa kumetokea taasisi ya Jumuiya ya Hifadhi ya Ziwa Burunge (JUHIBU) imeingia mkataba na viongozi wa vijiji kwa lengo la kuhifadhi vyanzo vya maji lakini malengo hayo wamegeuzwa na kuchukua ardhi yote ambayo kuna mashamba na makazi.
Kiongozi wa wananchi hao Bw. Sule alisema wananchi wa vijiji hivyo wananyanyasika kwa kufukuzwa katika maeneo yao ya asili kama wanyama wa porini na kutozwa faini ya mifugo inayonekana maeneo yao wanayamiliki kihalali na kuyalipia ushuru lakini kwa sasa hawatambuliki.
Alisema vijiji vyote kumi vya Maweni, Magara, Kisangani, Mwada, Mbuyani, Manyara,Mdori,Magugu, Mapea na Kambi ya Fisi wamekuwa wakitozwa faini ya sh. 10,000 kila ngombe mmoja anayekutwa katika maeneo ambayo wameyapima kutoka kwa wananchi bila kuwataarifu ni kwa ajili ya matumizi gani.
Bw. Sule aliendelea kusema nyumba zao zimevunjwa,mashamba yameharibiwa,makaburi yameondoshwa na ardhi hiyo kupimwa upya na kuwekwa alama za kuhalalisha “Bicons” na kuzuzuia wananchi wasisogee eneo hilo.
Alisema wananchi hao wanafahamu kuwa sheria ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999 namba 5 inasema mamlaka yoyote inapotaka kuchukua ardhi inayokaliwa au kutumiwa na mtu au watu “uhawilishaji” wanastahili kulipwa fidia stahili.
“Kinachofanywa na viongozi wa vijiji vyetu kushirikiana na JUHIBU ni ubabe na unyama ulijaa unyanyasaji kwani wameweka utu,sheria na haki ya mtanzania kuishi kewa amani haipo tena” alisema BW. Sule.
Alisema kabla ya kufikisha malalamiko yao kwa Waziri Profesa Tibaijuka waliwahi kufikisha malalamiko yao kwa viongozi wa ngazi ya Tarafa,wilaya na Mkoa wa Manyara lakini hakuna hatua iliyowahi kuchukuliwa kumaliza mtafaruku au mgogoro huo ambao umechukua muda mrefu.
Bw. Sule alisema wananchi hao wanaishi maisha magumu na kulazimika kuwa kama wakimbizi ndani ya nchi yao,hivyo wanaiomba serikali kama inataka wananchi hao waondoke ili kupisha wawekezaji basi wanaomba walipwe fidia stahili.
Katika barua hiyo waliomwandikia Waziri wa Ardhi yumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Tibaijuka wananchi hao walisema sheria zikifuatwa na wananchi kuelimishwa kusudio la Serikali kuhusu ardhi yao wao wako tayari kuhama lakini kama itafanywa kiujanja ujanja hawako tayari kuhama.
mwisho
No comments:
Post a Comment