TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION
TANGAZO SHIWATA
Tuesday, 30 July 2013
Wakuu wa wilaya Chemba,Kondoa wageuka mbogo
Na Eligius Gutta,Kondoa
WAKUU wa wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma wamecharuka kuhakikisha kuwa watendaji wa vijiji na kata wanawajibika ipasavyo katika kazi zao kwa kuwakamata wale wote ambao wanazembea kazi zao.
Matukio ya hivi karibuni ya wakuu hao wa wilaya za Chemba na Kondoa yametokea wakati wakuu hao wa wilaya hizo walipoagiza kuandaliwa kwa mikutano kwa ajili ya kuzungumza na wananchi lakini kwa uzembe mikutano hiyo haikufanyika na wao kuamua kuwakamata watendaji wa maeneo husika.
Katika wilaya ya Chemba mkuu wa wilaya hiyo Isack Francis alilazimika kumtia ndani mtendaji wa kata ya Ovada , Bw. Simon Nyang'ombe baada ya kutotimiza wajibu wake wa kusimamia ufyatuaji wa matofali kwa ajili ya ujenzi wa maabara na maktaba katika eneo lake.
Mjini Kondoa mkuu wa wilaya hiyo Omary Kwaangw jana(juzi)alilazimika kuwakamata watendaji wa kijiji cha Kondoa mjini na wa kata ambao majina yao hayakufahamika mara moja na kuwaweka chini ya ulinzi kwenye kituo cha polisi kutokana na kukwamisha mkutano ambao alitegemea azungumze na wananchi kuhamasisha maendeleo.
Kwa maelezo ya watendaji hao walidai kuwa walialika mikutano hiyo lakini wananch ndio hawakuhudhuria jambo ambalo mkuu wa wilaya ya Kondoa Bw. Kwaangw kuona ni uzembe katika ualikaji wa mkutano kwani kama taarifa zingewafikia kikamilifu wasingeacha kuhudhuria.
Sakata hilo la wakuu wa wilaya za Chemba na Kondoa limekuja siku chache baada ya Halmashauri ya Kondoa na Chemba kutengana rasmi Julai 19 wakati wa kikao cha baraza la halmashauri ya Kondoa ambapo Chemba nao waliunda uongozi wa halmashauri hiyo na kutambulishwa kwa wakuu wa idara za serikali na Kaimu Mkurugenzi Bw. George Pangawe kabla anayekusudiwa hajawasili.
Wakuu hao wa wilaya wakiunga mkono hotuba ya mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Rehema Nchimbi kuwa uanzishwaji wa halmashauri lengo lake ni kuwatumikia wananchi,walisema kuwa hawatakuwa tayari kumwonea haya kiongozi yeyote au mtendaji wa serikali katika maeneo yao ambaye atakuwa mzembe.
Walisema wananchi wanachotegemea ni maendeleo nA si siasa japo siasa ni sehemu ya maisha lakini itumike si kuharibu bali kuhamasisha maendeleo ya wananchi.
MWISHO.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment