TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Sunday, 7 July 2013

TABORA MARATHON YAFANA



Mgeni rasmi katika mbio za Tabora Marathon 2013, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini, Suleiman Kumchaya, akimkabidhi zawadi ya kitita cha sh 100,000 mshindi wa mbio za Kilomita 15, Grace Jackson.
Mgeni rasmi katika mbio za Tabora Marathon 2013, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini, Suleiman Kumchaya, akimvisha medali mshindi wa mbio za Kilomita 15.

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI mkoani Tabora imepongeza mashindano ya Tabora Marathon kufanikiwa kwa kiasi kikubwa na kwamba itakuwa bega kwa bega katika mashindano yajayo ya mwaka 2014.

Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini (DC), Suleiman Kumchaya, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi kwenye mbio hizo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Fatma Mwassa, alitoa pongezi hizo kwenye kilele cha mbio hizo zilizomalizikia kwenye viwanja vya taasisi mjini hapa.

Kumchaya alisema, amefarijika sana kuona vijana,wazee na watoto wamejitokeza kwa wingi kushiriki mbio za Tabora Marathon.

Hata hivyo aliwashauri washiriki wote kuunda vikundi kwenye maeneo yao ili wanapopata muda wanafanya mazoezi ya riadha na hata mashindano yatakapokuja mwakani wanakuwa fiti kimwili.

Kumchaya aliwaasa viongozi wa riadha mkoa wa Tabora, RITAM kwa kushirikiana na Kamati ya Tabora Marathon, kuanza maandalizi ya mbio za 2014,na baada ya kikao cha tathimini, wahakikishe wanakutana naye ofisini kwake kuweka mambo sawa kwa mbio zijazo.

Katika hatua nyingine serikali iliwapongeza wadau walijitokeza katika michango yao,kuwa serikali itandaa barua za kuwatambua wote kama shukrani kwao.

Wafadhili waliochangia kufanikisha mbio hizo ni Vodacom Tanzania, Filbert Bayi Foundation, mwanariadha wa kike, Banuelia Brighton, Meneja mfuko wa taifa wa bima ya afya Kanda ya Magharibi, Emmanuel Aidan, kampuni ya Tumbaku, ATTT, Mkurugenzi wa GONALLA Phamacy, Godbless Mafole, Posta, NMB, TRA NHC, MVP, Platnum Credit.

Tabora Marathon 2013, ilishirikisha mbio za Nusu Marathon Kilomita 21 kwa wanaume, Kilomita 15 kwa wanawake na Kilomita 5 kwa watoto na wazima.

Katika kilomita 21, mshindi wa kwanza aliibuka Tabu Mwandu aliyetumia saa 1:10.35 aliyezawadiwa kitita cha sh 100,000, kikombe na medali ya dhahabu, wa pili Dickson Mkami saa 1:13.18 na kujipatia sh 70,000 medali ya fedha huku nafasi ya tatu ikienda kwa Francis Jombe aliyetumia saa 1:14.36 na kuzawadiwa sh 60,000 na medali ya shaba.

Aidha kilomita 15 wanawake, Grace Jackson alishinda akitumia dakika 55:33.06 na kuzawadiwa sh 100,000, medali ya dhahabu na kikombe, wa pili Maombi Elisha dakika 58:52.01 na kuzawadiwa sh 70,000 na medali ya fedha huku nafasi ya tatu ikienda kwa Naomi Samweli aliyetumia saa 1:00.05 aliyejipoza kwa sh 60,000 na medaliya shaba.

Washindi wa nne na tano kila upande walizawadiwa sh 20,000 kila mmoja huku wa sita hadi wa kumi wakijipoza kwa sh 15,000 kila mmoja.

Kwa kilomita 5 wanaume wa kwanza aliibuka Robert Mayala wa pili ni Joseph Kimatile na kufuatiwa na Rashid Malugu waliopata medali za dhahabu, fedha na shaba.

Upande wa wanawake kilomita tano ni Getruda Musa wa pili Sara Lyimo na Asha Seleman ambao nao walipata medali, huku mkimbiaji mwenye umri mkubwa Msese Said (65), Msese Said akipata fedha sh 17,000 kutoka kwa akiwamo DC Kumchaya.

No comments:

Post a Comment