Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Kilimo, Adam Kighoma Malima atakuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Wasanii Mastaa litakalofanyika Juni 29, mwaka huu kwenye kijiji cha Mwanzega, Mkuranga mkoa wa Pwani.
Akizungumza na viongozi wa Mtandao wa Wasanii (SHIWATA) mjini Dodoma katika vikao vya Bunge vinavyoendelea, Malima alisema amekubali kuwa mgeni rasmi vile vile tukio hilo linafanyika katika jimbo lake la uchaguzi la Mkuranga.
Mwenyekiti wa SHIWATA, Caasim Taalib alisema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri na kuongeza kuwa kutakuwa na matukio ya wanachama kukabidhiwa nyumba zao kwa wale waliomaliza michango yao akiwemo mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars, Jellah Mtagwa atakabidhiwa nyumba yake.
Alisema katika tamasha hilo Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan atakabidhiwa kadi ya kujiunga na Mtandao wa Wasanii sambamba na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida.
Mwenyekiti Taalib alisema ahadi ya Bw. Madabida kuwa taasisi yake itawakopesha wasanii sh. Bil. 7 kwa ajili ya kuendeleza sanaa na ujenzi wa nyumba za makazi, mpango huo utaanza kutekelezwa kwa awamu ya kwanza.
Alisema wabunge mbalimbali wamealikwa kuhudhuria tamasha hilo akiwemo mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu na wabunge wengine ni John Mnyika wa Ubungo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, na Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR- Mageuzi , James Mbatia.
Alisema mtandao wa SHIWATA ambao umekuwa ukiandaa matamasha ya wasanii kila mwezi limepeleka tamasha la Juni kwenda wilaya ya Mkuranga ambako ndiko zinakojengwa nyumba zao katika kijiji cha Mwanzega-Kimbili ambako mpaka sasa watu nane watakabidhiwa nyumba zao.
Wasanii 400 kutoka vikundi mbalimbali vikiwemo vya mkoa wa Pwani wanatarajiwa kushiriki katika tamasha hilo .
mwisho
No comments:
Post a Comment