Majambazi yaua polisi Dar
Peter Mwenda
POLISI mmoja ameuwa na wengine wawili kujeruhiwa baada ya kupigwa risasi na majambazi yaliyokuwa yakifukuzwa na polisi.
Katika tukio hilo raia mmoja ambaye alikuwa akipita njia naye alijeruhiwa kwa risasi mkononi na wamelazwa hospitali wakiendelea na matibabu.
Kaimu mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke Dkt. Isdory Kiwale akizungumza na majira alisema amepokea majeruhi watatu na maiti mmoja.
Alisema kati ya majeruhi hao wawili kati yao ni askari polisi na mmoja ni raiamkazi wa Kiwalani.
Dkt.Kiwale alisema amepokea mwili wa marehemu ambaye ni askari mwenye namba G.2641 PC Mwinyi Juma ambaye alipigwa risasi kichwani na kufariki papo hapo.
Alisema majeruhi ambaye ni askari polisi mwenye namba G.2461 PC Jafari Lameck aliyevunjika mguu wa kushoto amehamishiwa kitengo cha Mifupa (MOI) cha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Alisema majeruhi Lameck amehamishwa Moi ili kutoa risasi ambayo imeshindwa kuonekana kwa haraka.
Dkt. Kiwale alisema majeruhi wawili wamelazwa wodi namba 7 kwenye hospitali hiyo na wanaendelea na matibabu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bw. Ahmed Msangi akizungumza na waandishi wa habari jana jioni baada ya tukio hilo alisema askari walioshambuliwa na majambazi walikuwa katika sare za polisi wakiwa katika doria ya kawaida eneo la Mchicha barabara ya Nyerere.
"Wakati makachero wetu wakiwafuatilia, majambazi hao walipohisi wanafutiliwa walishtuka na kuzidisha mwendo wa gari lao na kuchepuka kufuata njia ya vumbi eneo la Mchicha, wakifyatua ovyo risasi, ghafla waliwakuta askari wa doria wakiwa katika sare za kazi za kawaida na kuwafyatulia risasi" alisema Kamanda Msangi.
Alisema majambazi hao wakiwa katika gari dogo aina ya Toyota Carina lenye namba za usajili T319 BSY likiwa na vioo vya giza likiendeshwa kwa mwendo wa kasi lilitokomea.
Alisema baada ya tukio hilo msako mkali ulianza na muda mfupi walifanikiwa kupata gari lililokuwa likitumiwa na majambazi hao na watu watani wamekamatwa.
Kamanda Msangi alisema Jeshi la Polisi linaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano ili kuwakamata majambazi waliofanya tukio la mauaji.
mwisho
No comments:
Post a Comment