UMEME MTWARA, LINDI SH 99,000
Na Peter Mwenda, Mtwara
WIZARA ya Nishati na Madini imetoa kibali kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kanda ya Mtwara lianze kutekeleza ahadi ya kupunguza gharama za kufunga umeme kwa wakazi mikoa ya kanda ya kusini kwa Sh 99,000 kutoka gharama ya sh. 450,000 ya kuunganisha nishati hiyo.
Meneja Mkuu wa Kituo cha Uzalishaji umeme kwa kutumia gesi, Mkurunguma Chinumba akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea mitambo ya uzalishaji umeme ya kituo hicho jana alisema punguzo hilo linafikia kikomo Desemba mwaka huu.
Alisema serikali imetoa punguzo hilo kwa wakazi wa mkoa wa Lindi na Mtwara ambao wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa ni ya muda mfupi.
“Jana (juzi) tupokea waraka maalum unaotutaka kuanza kutekeleza ahadi hiyo kwa wakazi wa mikoa ya Mtwara na Lindi, kwa maana hiyo kuanzia sasa wakazi hawa watapatiwa umeme kwa gharama za bei nafu kabisa.
“Kama ilivyotangazwa hapo awali, ni kwamba sasa watafungiwa na kupatiwa huduma zote za umeme kwa gharama ya Sh 99,000 pekee, punguzo hili litadumu kuanzia sasa hadi Desemba mwaka huu, ndio maana natoa wito kwa wakazi wetu kuchangamkia fursa hii ya kipekee.
“Fursa hii maalum kwa wakazi wa mkoa huu kwa sababu kama mnavyofahamu, umeme unaozalishwa katika Kituo hiki cha Mtwara unatokana na gesi ambayo inachimbwa hapa hapa.
“Lakini pia kituo hiki sasa kinauwezo wa kuzalisha umeme wa Megawati 18, wakati mikoa ya Lindi na Mtwara inatumia kiasi cha umeme Megawati 12.5, kwa maana hiyo umeme upo wa kutosheleza na kubaki,” alisema.
Aidha alisema kituo hicho kipo katika mikakati kabambe ya kupanua wigo wa uzalishaji pamoja na miundombinu yake kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wa viwanda mbalimbali.
“Kiwanda cha saruji, kiwanda cha mbolea pamoja na viwanda vingine ambavyo tunatarajia vitakuja kufunguliwa hapa Mtwara, kwa maana hiyo vitatumia umeme unaozalishwa na kituo hiki ndio maana tumejiopanga kuzidisha uzalishaji.
“Kwa sababu kama mlivyoona kituo hiki kinapokea bomba la gesi lenye futi za ujazo milioni 10, lakini kutokana na uwezo wetu kwa sasa tunatumia futi za ujazo milioni mbili pekee, ndio maana tunaona kuwa kuna kiasi kikubwa sana kinabaki,” alisema.
Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Fadhil Kilewo alisema punguzo hilo halihusu bei ya kununua umeme majumbani ambayo ni sh. 125 kwa uniti moja kwa nchi nzima
No comments:
Post a Comment