TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Wednesday, 26 September 2012

Mbunge Vullu akamatwa akitoa rushwa Kisarawe

Na Peter Mwenda, Kisarawe

MBUNGE wa Viti Maalum CCM mkoa wa Pwani, Bi. Zainab Vullu amekamatwa na kuhojiwa na Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) akidaiwa kugawa fedha kwa wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) wilaya ya Kisarawe.

Taarifa za awali zinasema kuwa Mbunge Vullu alikamatwa na wenzake wawili Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Kisarawe Bi. Asia Madina na Katibu wa UWT wa wilaya Bi. Mwajuma Mombwe.

Tukio hilo lilitokea Jumanne saa 11 jioni baada ya kumalizika kwa kikao cha Baraza Kuu la UWT wilaya ya Kisarawe kilichohudhuriwa na wajumbe 49 kutoka Kata 15 za Wilaya, maofisa wa PCCB walipovamia kikao hicho na kukamata kitita sh. 550,000 ambazo alikuwa akigawa Bi. Madina kwa wajumbe.

Maofisa hao waliwakamata viongozi hao yaani Mbunge Vullu,Mwenyekiti wa UWT wilaya Bi. Asia na Katibu wake Bi. Mombwe na kushikilia fedha alizokuwa nazo Bi. Madina akigawa kwa wajumbe na nyaraka zote walizokuwa nazo mezani zilichukuwa na TAKUKURU.

Baada ya tukio hilo watuhumiwa hao walikubali kutii amri ya kwenda TAKUKURU ambako walikaa kwa muda na baadaye kupewa taarifa kuwa waripoti siku ya pili (jana) kwa mahojiano zaidi.

Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Pwani, Bi. Joyce Shirima alikiri kutokea tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa zaidi baada ya uchaguzi kukamilika.

"Najua unataka kujua habari za Kisarawe lakini bado uchunguzi unaendelea kufanyika na kesho (leo) nitatoa taarifa kamili" alisema Kamanda wa Takukuru Bi. Joyce.

Akizungumza na waandishi wa habari Bi. Vullu alikana kukamatwa na rushwa akidai kuwa yeye alikuwa mjumbe mwalikwa kama wengine hivyo alistahili kupata posho na chakula kama wengine.

"Sina mahala popote ambapo mimi nimehojiwa wala kukamatwa na TAKUKURU wala hakuna mahala popote panaonesha nimehojiwa'Alisema Bi. Vullu.

Alisema yeye alistahili kuhudhuria kikao cha Baraza la UWT wilaya kwa kuwa ni mjumbe halali pia ni Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Pwani na kuongeza kuwa hakukutwa akigawa fedha.

Bi. Vullu alidai kuwa kikao hicho kilikuwa na usahihi wa kugawa posho kama vinavyofanyika vikao vingine vya chama anashangaa kuona TAKUKURU iliwakamata.

Naye Bi. Madina aliyekamatwa akigawa fedha hizo alikiri kukutwa na sh. 550,000 ambazo alikuwa akigawa kwa majumbe na kuongeza kuwa azikusanya kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo waheshimiwa mbalimbali na madiwani ambako yeye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe na Diwani wa Viti maalum.

"Vikao vyote tunavyofanya hapa viwe vya chama viwe vya Jumuia hutolewa posho kwa sababu wajumbe wanatoka mbali na kuongeza kuwa sh. 10,000 ni nauli ya kumtoa mjumbe  katika kata yake kufika kuhudhuria kikao" alidai Bi. Madina.

mwisho







No comments:

Post a Comment