TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Tuesday, 12 June 2012

Viongozi wa dini wabaini upotevu trilioni 3.2 kila mwaka nchini

Na Peter Mwenda

VIONGOZI wa Dini ya Kiislamu na Wakristo nchini wamebaini upotevu wa dola za Marekani Bilioni Moja (sawa na Trilioni 3) kila mwaka kutokana na ukwepaji kulipa kodi,utoroshwaji wa mali na misamaha ya kodi kwa wawekezaji kama kivutio.

Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Dini ya Haki za Kijamii, Uchumi na Hifadhi ya Uumbaji Tanzania (HUJUUTA), Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tabora, Paul Ruzoka alisema fedha zinazopotea ni 1/6 ya bajeti ya Serikali.

"Kama mapato hayo yangetumika kugharamia elimu, ingekuwa mara mbili ya bajeti ya Wizara ya Elimu, hali kadhalika kwa Wizara ya Afya na Sera za Kilimo Kwanza ingekuwa mara tatu ya ilivyo sasa" alisema Askofu Ruzoka.

Alisema sababu za upotevu wa mapato ya taifa ni sera mbovu za ukusanyaji mapato ambako misamaha ya kodi kwa Makampuni inasababisha nchi kupoteza dola za Marekani milioni 288, utoroshwaji wa mali ambazo ni fedha na rasilimali nyinginezo ni dola za Marekani mil. 300.

"Fedha hizi ni zile zinatokana na mwingiliano wa shughuli za makampuni yaliyo katika nchi zaidi ya moja" alisema Askofu Ruzoka ambaye Kamati yake inaundwa na Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

Askofu Ruzoka alisema ili kuinusuru Tanzania kutokana na hasara hiyo ipo haja ya kuwa na mikakati mipya na dhahiri ya ukusanyaji mapato kutoka kwa makampuni yanayoendesha biashara nchini kwa kuweka mfumo madhubuti utakaohakikishia Serikali mapato ya kutosha kuendesha shughuli zake badala ya kutegemea mashirika ya fedha na Serikali ya nchi hisani.

Alisema ushauri mwingine kwa Serikali ni kuwa ipange namna ya kuongeza mapato yake wakati wa kujadili bajeti ya 2012/2013 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano lililoanza jana Dodoma na itazame upya utaratibu wa kuvutia wawekezaji na makampuni katika kutoa misamaha ya kodi ili kubaini namna ya kuipunguza kama siyo kuiondoa kabisa.

Pia wameishauri Serikali kila mwaka ijiwekee utaratibu wa kutathimini gharama za matumizi yatokanayo na misamaha ya kodi ili kujua bayana walionufaika na mtindo huo na kuhakikisha mikataba na makubaliano ya wawekezaji, makampuni yanayomiliki migodi mbalimbali unajulikana na iko wazi zaidi na inazingatia Sheria za Tanzania kwa faida ya wananchi.

Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa viongozi wa dini wanao wasiwasi juu ya hali ilivyo na kusikitishwa kuona zawadi waliyonayo watanzania ya utajiri wa rasilimali zilizotolewa na Mungu zinatoweka kutokana na kutokuwa na Sera madhubuti zenye kudhibiti ukwepaji wa kulipa kodi, utoroshaji wa mali na misamaha ya kodi kwa makampuni.

"Sera ya mafuta na Nishati ya gesi inatazamwe upya ikiwa ni pamoja na kutambua na kuweka tahadhari katika uchimbaji wa Urani" alisema Askofu Ruzoka.

Pia Kamati hiyo imeitaka Serikali itamke mwananchi wa kawaida wananufaikaje na utafutaji wa mafuta na nishati zenye kuambatana na zao hilo na iwe makini kusimamia kwa ustawi wa taifa.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) Dkt. Prosper Ngowi aliyeongoza utafiti huo alisema katika utafiti wao wamegundua nyufa nyingi zinazosababisha serikali kukosa mapato.

Alisema ilikuwa kazi ngumu kupata ushirikiano wa kupata taarifa za upotevu wa fedha hizo mojawapo ni makampuni kununua rasilimali kwa bei ya chini na kuzuiza kwao kwa bei ya chini zaidi ambako mwisho wa siku makampuni hayo kuonekana yanapata hasara kutumia njia hiyo jumla ya dola bil. 2.5 zimetoroshwa.

Alisema dola mil. 435 zinapotea kila mwaka kutokana na kuvutia wawekezaji na taarifa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilibaini kuwa migodi mikubwa Tanzania haijawahi kulipa kodi hadi kufikia mwaka 2008.

Alisema watanzania wamekuwa wema kupita kiasi na wanaolipa kodi kubwa kwenye migodi ni wafanyakazi wanaolipa kodi ya Lipa Kadri Unavyolipwa (PAYEE) si wamiliki wa migodi mikubwa.

Dkt. Ngowi alisema fedha zilizopotea kwa njia ya misamaha ya kodi mwaka 2009/2010 ni sh. trilioni 3.2 ambazo ni sawa na fedha zilizotolewa na wahisani kwenye bajeti hivyo kama makusanyo yangedhibitiwa kusingekuwa na haja ya kuomba fedha kutoka nje.

Alisema katika misamaha hiyo mashirika ya dini yanapata asilimia 0.06 lakini wawekezaji wanapata kiasi kikubwa ambacho ni kichocheo cha kuchukua rasilimali za watanzania.

Katika mkutano huo ambao kwa upande wa waislamu uliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Hassan Fereji, Shekhe Waziri Seif aliyemwakilisha Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Alhadi Salum, CCT iliwakilishwa na Mchungaji Leonard  Mtaita.

mwisho

No comments:

Post a Comment