TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Sunday, 10 June 2012

TENGA AAGIZA UCHUNGUZI UFANYIKE SAKATA LA YONDANI KUONDOKA KAMBI YA STARS KWENDA KUSAINI MKATABA YANGA





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KLABU ya soka ya Simba imepokea kwa furaha taarifa kwamba Rais wa Shirikisho la Mpira was Miguu Tanzania (TFF), Leodger Chila Tenga, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusiana na namna mchezaji wa Simba na Taifa Stars, Kelvin Patrick Yondani, alivyoondoka kambini usiku wa kuamkia Juni 7 mwaka huu.
Katika barua ambayo Tenga ameiandikia Simba, ameahidi kwamba uchunguzi utafanyika katika maeneo makuu mawili. Mosi, iwapo ni kweli Yondani aliondoka kambini usiku, pili iwapo aliondoka kwa ruhusa maalumu au alitoroka. 
Tenga ameahidi kwamba kama ikibainika kwamba aliondoka bila ruhusa, basi hatua zitachukuliwa kwa wote waliohusika chini ya taratibu za maadili kwa wachezaji  (Players Code of Conduct).
Kutokana na kauli hiyo ya Tenga, uongozi wa Simba umeamua sasa kwamba hautozungumza lolote kuhusiana na masuala ya Yondani. Tayari timu imewasilisha vielelezo vyake TFF na kote kwingine ambako suala hilo linaweza kufika. Kilichobaki sasa ni kusubiri vyombo husika vifanye kazi yake.
Simba SC inapenda kuchukua nafasi hii kuwaomba wapenzi na wanachama wake kutulia na kutobabaishwa na taarifa za wachezaji wake kusajiliwa na timu nyingine. 
Kwa sasa Simba inaendelea na mikakati yake ya usajili unaokidhi vigezo vya kimataifa ambao ulisababisha msimu uliopita itwae ubingwa wa Tanzania na kuifunga YANGA goli 5-0 !
Simba si timu ya maneno mengi kwenye usajili bali ni vitendo. 
Tunaomba wanachama wetu watulie na mara ifikapo tareje 15 Juni mwaka huu, mbivu na mbichi zote zitajulikana. Siku hiyo, Simba itatangaza wachezaji wake wote iliyowasajili na iliyowaacha. 
Simba ndiyo mabingwa wa Tanzania na washabiki wake wanatakiwa kutembea vifua mbele popote pale walipo na wasichanganywe na taarifa za pembeni. 
Uongozi wa Simba uko makini na unafanya kazi zake kisayansi.

Imetolewa na 

Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC

KUELEKEA MCHEZO WA GAMBIA KESHO-POULSEN ALIA NA TFF


TIMU ya soka ya Taifa ‘Kili Taifa Stars’ kesho inashuka katika dimba la Taifa jijini Dar es Salam kukwaana na Gambia ‘The Scorpions’ katika mchezo wa mchujo wa kuwania kucheza fainali za kombe la dunia 2014 zitakazopigwa nchini Brazil. 
Akizungumza na waandishi wa habari,kocha mkuu wa Stars,  Mdenmark Kim Poulsen  alisema kikosi kikosi chake kipo katika hali nzuri ya kimchezo ambao anaamini utakuwa na upinzani mkubwa.
 Hata hivyo, Poulsen alisikitishwa TFF kutompatia  DVD za mechi za Gambia ili iweze kuwasaidia katika maandalizi ya mchezo wa kesho na kuongeza kuwa hii ni mara ya pili kushindwa kupatiwa DVD hizo ambapo awali ilikuwa katika mchezo dhidi ya Ivory Coast ambapo Stars ililala mabao 2-0.
 “Pamoja na kuzikosa DVD hizo nimekiandaa kikosi changu kukabiliana na Gambia ambapo naamini watatumia vizuri uwanja wa nyumbani kwa kushinda mabao mengi,”alisema.
 Poulsen aliongeza kuwa wachezaji wake wapo katika hali nzuri isipokuwa Nurdin bakari, huku kiungo mshambuliaji Haruna Moshi ‘Boban’ aliyekuwa majeruhi hali yake ikiimarika na huenda leo akampanga dimbani.
 Hata hivyo mchezo wa kesho  unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa na hasa ikizingatiwa kila timu inahitaji ushindi ambapo Gambia ilitoka sare ya bao 1-1  Morocco na Morocco katika mchezo wao ulipigwa nyumbani wiki iliyopita. 
Kocha wa Gambia, Mtaliano Luciano Machini akizungumza jana katika mazoezi yao kwenye uwanja wa Karume, alisema  itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao ni wazuri na wana kasi uwanjani.
 Mchezo huo utakapigwa kuanzia saa 10.00 jioni na kuchezeshwa na waamuzi kutoka nchini Zimbabwe,  Ruzive Ruzive akisaidiwa na Salani Ncube na Edger Rumeck ambapo tiketi zimeanza kuuzwa leo  katika vituo mbalimbali huku kesho  zoezi hilo litahamia uwanja wa Taifa kuazia saa 6 mchana.
 Viingilio katika mchezo huo ni  sh.3,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, huku sh.5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, wakati VIP C watalipa sh. 10,000 ,  VIP B watalipa sh. 20,000 na watakaokaa VIP A watalipa  sh. 30,000.

No comments:

Post a Comment