TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Sunday, 10 June 2012

Mbwa ni mlinzi namba moja-DC Amina Masenza

Na Tamimu Adam Jeshi la Polisi Mwanza

WAKURUGENZI wa Kampuni binafsi za ulinzi kote nchini wametakiwa kuwatumia mbwa waliopata mafunzo maalumu katika kuzuia na kubaini wahalifu na uhalifu katika maeneo yao ya kazi ili kuimarisha ulinzi wakati wote wanapokuwa katika malindo yao na kuepusha walinzi wao kuporwa silaha au kuuawa na wahalifu.

Hayo yalisemwa na mkuu wa wilaya ya Ilemela Bi. Amina Masenza wakati akizindua klabu ya Mbwa mlinzi jijini Mwanza ambayo ilianzishwa kwa madhumuni ya kuwapatia mbwa mafunzo maalumu ili waweze kuwasaidia katika kuimarisha ulinzi katika makazi watu na kutekeleza kwa vitendo dhana ya Polisi jamii na Ulinzi shirikishi.

Bi. Masenza alisema mbwa ni mlinzi mwaminifu sana katika kubaini na kuwafichua wahalifu mahali popote hivyo ni vizuri makampuni binafsi yakaweka kipaumbele kutumia Mbwa wenye mafunzo ili kuhakikisha usalama wa walinzi wao, pamoja na raia unaimarika.

Alisema klabu hiyo ni muhimu sana hasa katika kipindi hiki na inapaswa kuwa endelevu na inashiriki mashindano na maonesho mbalimbali yanayoandaliwa hapa nchini na kwingineko ili kuweza kulitangaza jiji la Mwanza katika masuala ya kiulinzi na usalama.

Kwa upande wake Mlezi wa klabu hiyo  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishina Msaidizi wa Polisi Liberatus Barro alisema mbwa ni mlinzi mzuri kwa kuwa hawezi kula njama na wahalifu wala kuomba au kupokea rushwa hivyo ni vizuri wanachama na watu wengine kutumia fursa hiyo ili waweze kujua namna ya kuwatunza mbwa kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

Naye Kamanda wa Kikosi cha Mbwa na Farasi Mkoa wa Mwanza Mrakibu Msaidizi wa Polisi Namsemba Mwakatobe alisema wakazi wote wa Mwanza wanaomiliki Mbwa wanaruhusiwa kujiunga na klabu hiyo na kuleta Mbwa wao ili waweze kupata mafunzo.

No comments:

Post a Comment