TANGAZO ISERESPORTS COLLECTION

TANGAZO SHIWATA

Thursday, 12 April 2012

Mahiza awacharukia watoa huduma, asema wanaikwamisha NHIF



Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Kiwenge akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambay alifungua mkutano wa wadau wa mfuko huo wa Bima ya Afya mjini Kibaha leo

Ofisa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa mfuko huo, Grace Michael akiratibu mkutano wa wadau wa NHIF Mkoa wa Pwani leo, mjini Kibaha.
Baadhi ya wadau wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza na viongozi wa NHIF

Wanahabari wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa NHIF pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mahiza
Mahiza akizungumza na wanahabari baada ya kufungua mkutano huo
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NHIF, Eugen Mkongoti akielezea jinsi wadau wa mfuko huo na hasa wanachama wanavyonufaika na mfuko huo na ule wa Mfuko wa Afya ya Jamii.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa NHIF, Beatus akiwahamasisha wadau kujiunga na mfuko huo ili wanufaike nao
Mahiza akiagana na Mkurugenzi wa NHIF, Humba. Kushoto ni Grace Michael ambaye ni Ofisa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa mfuko huo



*Aonya kutumia muda kupiga soga badala ya huduma
Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza ameonesha kukerwa na tabia ya baadhi ya watoa huduma za afya kwa kushindwa kutoa huduma bora kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na wananchi kwa ujumla huku wakitumia muda wao mwingi kupiga soga ama kunywa chai maofisini.
Amesema kuwa haki inakwenda na wajibu hivyo watoa huduma wanatakiwa kutanguliza upendo kwa wananchi kwani wana haki ya kupata huduma kwa wakati wanapokwenda hospitali ama kwenye vituo vya afya.
Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Pwani,Mahiza alisema kuna baadhi ya watoa huduma katika sekta ya afya wanangalia zaidi maslahi yao kuliko kuangalia majukumu yao hali inayokwamisha wananchi kuona umuhimu wa kujiunga na utaratibu wa bima za afya.
Alisema imefika mahali watoa huduma wanajifungia ofisini kupiga soga ama kunywa chai wakati wagonjwa wanateseka kwa kupanga foleni kusubiri huduma kitu ambacho amesema hayuko tayari kukivumilia.
"Kuna baadhi ya watoa huduma wao hawaoni umuhimu wa kuhudumia wagonjwa. Wagonjwa wamepanga foleni nje wao wanajifungua ofisini wanakunywa chai.
"Hapana jamani naomba tubadilike, wapo baadhi ya watendaji katika sekta ya afya wanafanya kazi nzuri ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati.Hivyo wale ambao wanaona wao ni miongoni mwa wale wasiopenda kutoa huduma wabadilike au waache kazi kuliko kuendendelea kudharirisha wegonjwa,"alisema Mahiza.
Hata hivyo aliwaambia watendaji na watoa huduma wote wa Mkoa wa Pwani kutambua kuwa pamoja na kuwepo changamoto nyingi katika sekta ya afya bado wanatakiwa kutimiza majukumu yao ili hata wanapodai haki iwe ina maana zaidi.
Alisema kuwa kila kazi inachangamoto zake lakini bado kwa anayeifanya anayo nafasi ya kutambua kuwa kama anaona haimfai anaweza kutafuta kazi nyingine ya kufanya.
Aliongeza kuwa inawezekana baadhi yao wakaona anatumia lugha kali na kumtaka kuomba radhi kitu ambacho hatakifanya kwa kuwa ameamua kutoa dukuduku lake kwa kutaka mambo yaende sawa huku akiongeza kuwa Tanzania inajengwa na wananchi wote.
Alisema kuwa kuna baadhi ya watendaji utawasikia wakidai haki lakini ukiangalia majukumu yao hakuna kitu ambacho wanakifanya au kulingana na madai yao.
Akifafanua zaidi kuhusu sekta ya afya alisema kuwa kuna baadhi ya hospitali na vituo vya afya watoa huduma wake wanatoa huduma za matibabu kwa kumuangalia mtu alivyovaa jambo alilolikemea na kutaka lisionekane mkoani mwake.
"Kuna siku nilienda moja ya hospitali, nilipofika pale nikakuta kuna mgonjwa amekosa huduma kwa zaidi ya saa 12 tena amepata ajali.Kitanda alicholala hata shuka hajapewa.Lakini akaja mtu kwasababu tu fulani akafika na kupewa huduma.
"Kitendo cha kutoa huduma kwa kuangalia mgonjwa kavaa nini ama amepaka lip stick ya aina gani mdomo hii si sawa.Sote ni Watanzania tunahitaji kupata huduma iliyosawa. Kutoa huduma ya afya kwa kuangaliana usoni inawakatisha tamaa wananchi. Tubabadikike,"aliongeza.
Pia alisema katika kuhakikisha Mkoa wa Pwani unapiga hatua katika kutoa huduma za afya atahakikisha anafanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya afya na hospitali kwa kuenda bila kutumia gari ya Serikali.
Alisema amekuwa na kawaida ya kufanya ziara katika baadhi ya maeneo ya kiutendaji ili kuona mambo yanavyofanyika na ambayo amekuwa akiyakuta huko mengine hayaridhishi.
Pia alisema kuwa tatizo lingine ambalo limekuwa kero kwa wananchi ni kukosekana kwa dawa hata panaldo changamoto inayosababisha kikwazo kwa mfuko huo.
Alisema kuna tatizo upande wa MSD ambao ndiyo wanahusika na utoaji wa dawa na hata halmashauri inapopeleka orodha ya dawa na fedha bado wanashindwa kupewa kwa wakati hali ambayo inakatisha tamaa.
Alisema umefika wakati kwa MSD kutimiza majukumu yao na kuhakikisha halmashauri zinapotoa ombi la kupatiwa dawa wanapewa kwa wakati badala ya kushindwa kuwapatia ama kuwapa tofauti na mahitaji yao.
"Umefika wakati kwa watendaji na watumishi wa umma kutambua majukumu yao.Ili pale ambao wanasimama kudaia maslahi yao lakini pia wawe wametimiza majukumu yao ikiwa pamoja na kuhudumia wananchi wao.
Maendeleo yetu yatatokana na sisi wenyewe.Tanzania ndiyo nchi yetu hakuna nyingine.Unaweza kukuta nchi imeanza na T lakini haitakuwa Tanzania,"alisema Mahiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, alisema kuwa ili kuboresha huduma kwa wanachama wake, Mfuko unaandaa utaratibu wa kuwatumia madaktari bingwa ili wakatoe huduma kwa wanachama hasa walioko katika mikoa ya pembezoni.
Alisema Mfuko uko tayari kuhakikisha unabaoresha sekta ya afya kupitia fursa inazozitoa ikiwemo ya Mikopo ya Vifaa tiba na ukarabati wa majengo fursa inayolenga moja kwa moja kuwasaidia wananchi wote katika sekta ya afya.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unaendelea na mikutano yake katika mikoa mbalimbali ambapo kesho utakuwa na mkutano Mkoani Morogoro lengo ni kutoa elimu kwa umma ili kupanua wigo wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

No comments:

Post a Comment